BREAKING NEWS

[5]

ITUMIE VYEMA NEEMA YA UKUHANI -1



ITUMIE VYEMA NEEMA YA UKUHANI -1

Ufunuo 5;9-10
“Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Kwa Neema yake Mungu hapo tulipokuwa wafu kwasababu ya dhambi alitufufua pamoja na Kristo akisha kutusamehe dhambi zetu kwa damu yake,na kwa Neema yake kuu akatufanya Ufalme na Makuhani kwa Mungu.
Nafasi ya Ukuhani ni nafasi ambayo Mungu mwenyewe aliianzisha,kwa ajili ya kutengeneza mazingizingira ya yeye kukaa katika ya wanadamu.
Nafasi ya kikuhani ni nafasi ambayo kila mtu aliyempokea Yesu Kristo anapewa.Agano la kale Mungu alichagua Uzao wa Haruni pekee yake kusimama mbele zake katika nafasi ya Ukuhani lakini katika Agano bora (Agano jipya) kila aliyempokea Yesu amefanyika Kuhani mbele za Bwana,pasipo kujali kigezo cha Kabila,lugha,jamaa na taifa.

Mungu ni mwaminifu sana na analiheshimu sana Neno lake,Yeye mwenyewe ndiye aliyeanzisha Kiti cha Ukuhani,hivyo mtu yoyote anaposema na Mungu kutokea kwenye Nafasi ya Ukuhani,Mungu anaheshima sana maneno ya mtu huyo na maombi ya mtu huyo anayeomba kutoka kwenye kiti cha Ukuhani.Heshima hii sio kwasababu ya mtu bali ni kwasababu ya Nafasi ya Kikuhani ambayo anayeomba amesimama katika hiyo.

Waebrania 5; 4-6
“Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele Kwa mfano wa Melkizedeki”

Neno hili hapo juu linaonyesha wazi kuwa hakuna mtu awezaye kujifanya kuhani au kujipa Heshima hii ya Kikuhani mbele za Mungu.Heshima hii Hutoka kwa Mungu mwenyewe.Haruni alipewa Kiti na Mungu mwenyewe na Yesu pia.Vile Mungu mwenyewe ndiye anayempa Mtu Heshima hii ya Ukuhani inafanya nafasi hii Kikuhani kuwa ya Heshima sana mbele zake na Kumfanya Mungu kuheshimu sana Maombi yanayofanywa na mtu kama Kuhani juu ya familia,kanisa,ukoo,mkoa,nchi na dunia.Heshima iliyopo kwenye KITI/NAFASI ya Kikuhani ni Heshima aliyotangulia Mungu kuiweka mwenyewe kwenye Kiti hicho alipoamua kukiweka Kisimame mbele zake. Mtu anaposimama kwenye nafasi hii mbele za Mungu,anakuwa na Heshima ya kusikilizwa na Mungu kulingana na heshima ambayo Mungu mwenyewe aliiruhusu ikae juu ya kiti hiki mbele zake.Ni sawa na mtu akikuuliza swali hili,Hivi Mungu anaheshimu kwa kiwango gani nafasi ya Kuhani mbele zake..nawe ukamjibu kwa swali,,hivi Mungu aliweka heshima Kiasi gani kwenye Nafasi ya Ukuhani alipoamua Kuianzisha ili idumu mbele zake.? Heshima hii aliyoweka Mungu kwenye nafasi ya Kuhani ndio inayofanya Maombi yanayofanywa na  mtu yoyote anapokuwa amesimama kwenye nafasi hii yawe na Nguvu sana Mbele za Mungu.Kinachoyapa uzito mbele za Mungu maombi ya Kuhani ni Nafasi ya Kikuhani.

Mtu anaposimama mbele za Mungu kama Kuhani maombi yake yanakuwa na nguvu sana,pasipo kujali watu wamefanya uovu gani mbele za Mungu.Hesabu 16 Inaonyesha jinsi Mungu anavyoheshimu Nafasi ya Ukuhani na jinsi mtu anaposimama katika maombi kama Kuhani jinsi anavyoweza kuokoa nafsi za wengi hata kama ghadhabu ya Mungu ilikuwa imewaka juu yao.Israel walifanya jambo ambalo lilimkera sana Mungu na ghadhabu yake iliwaka na tauni ilikuwa inawaangamiza,Musa kwa kuijua nguvu ya Maombi ya Kuhani anamsihi Haruni kusimama mbele za Mungu kwaajili ya Israel ili Mungu awasamehe na Utaona jambo la ajabu sana Haruni aliposimama tu mbele za Mungu,Mungu alighairi hasira yake.Ni nafasi ya kikuhani pekee ambayo inaweza kumpa mtu nafasi ya kusimama mbele za Mungu mwenye ghadhabu na akaweza kuituliza ghadhabu hiyo na waliofanya uovu wakasamehewa.
Hesabu 16;44-48
“Naye Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi.
Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa Bwana; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu.
Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa.”

Mungu ameweka Neno la Upatanisho ndani ya kila Mwamini,ametupa Nafasi ya Heshima sana.Sio kwamba Mungu alimweshimu sana Haruni hata akaghairi uharibifu aliokusudia juu la kusanyiko hapana,Mungu alimweshimu Kuhani Haruni aliyesimama kwenye nafasi ya Ukuhani.
Kutokujua nguvu uliyonayo kama Kuhani mbele za Bwana inakufanya usitumie nguvu hiyo,Kukosa Ufahamu kunamfanya Adui aendelee kuangamiza familia yako wakati Mungu amekupa Heshima ya Kusimama mbele zake kwa ajili ya Familia yako.

Unaweza kuwa Kuhani lakini ukawa huna Fikra na nia anayotakiwa kuwa nayo kuhani.Hiyo ndiyo shida tuliyo nayo ndani ya Kanisa leo.Kama Kuhani wa Bwana yakupasa kufanya yafuatayo.

1.Vaa nia ya Upatanisho

Mungu alipoweka Ukuhani aliweka akiwa na Nia ya kuwa Kuhani atampatanisha Yeye na wanadamu wanapotenda dhambi.Hivyo Nia ya kuu ambayo kuhani anapaswa kuwa nayo ni Kupatanisha watu na Mungu,kupatanisha familia,ukoo,kabila, na hata  nchi na Mungu,kutengeneza mazingira ya amani kati ya Mungu na mwanadamu.
Israel walipotenda dhambi,walikuwa hawajamkosea Mungu tu,ila kosa lao lilikuwa Kumnung’unikia Musa na Haruni.Hivyo Musa angeweza kukaa kando na kuacha Mungu awaangamize Israel,ukizingatia walikuwa wamtendea uovu yeye na Haruni.Lakini Musa alikuwa ndani yake amevaa nia ya Upatanisho,nafsi za Israel zilikuwa na thamani mbele zake.Wakati Mungu anawaadhibu yeye alimsemesha Haruni kufanya Upatanisho kwa ajili yao.Nia hii ndiyo wengi ambao ni makuhani hawana,wameokoka bado wanania ile ya utu wa kale ya Adui mwombee njaa.Huwezi ukaingia kwenye Ofisi ya Ukuhani ukiwa umevaa fikra za utu wa kale ukaweza kufanya kazi.Kiti cha Ukuhani hakipo kwaajili ya kutoa Hukumu,Nafasi ya Ukuhani ni kwaajili ya Kuombea rehema na kuwapatanisha watu na Mungu ni seme hivi kuhani yoyote anatakiwa aione thamani ndani ya kila nafsi ya mtu awe mwenye dhambi au hana dhambi kama vile Mungu anavyoiona thamani ya nafsi ya mtu mbele zake, hapo ndipo Kuhani atafanikiwa sana kwenye nafasi yake.Musa aliona thamani kwa zile nafsi zilizokuwa zinaangamia,aliona thamani ya sura na mfano wa Mungu ndani ya wale watu ndio maana pamoja na kwamba walimtenda vibaya yeye aliweza kumsihii Haruni awaombee rehema.
Eliya alikuwa Kuhani, aliteketeza roho 100 kwa moto kutoka mbinguni,akaokoa roho 50 za watu waliokuja mbele zake kwa staili moja.Nini kilifanya wale 100 wa kwanza wakaangamia na hawa 50 wakapona? Thamani ya rohoi hizi 50.Hawa ndugu 50 walimsemesha Eliya maneno yaliyofunua macho ya Eliya kutazama Thamani za rohoi zao mbele zake.
9 Ndipo mfalme akatuma akida wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka.10 Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.11 Akatuma tena akida wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi.
 12 Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.13 Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako.14 Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. 2Wafalme 1;9-14.

Ni hatari sana kwa Kuhani kuacha kufanya Upatanisho kwa ajili ya familia na kuanza kuhukumu familia yako.Familia ikipigwa huwezi kuwa na Amani na furaha,usifikiri nchi kuwa chini na hasira ya Mungu wewe utakaa salama,maandiko yanasema katika amani ya nchi ndiko utakapopata amani yako.
Neema ya Yesu iwe juu yako,tutaendelea sehemu ya pili,endelea kufuatilia …..
ITUMIE VYEMA NEEMA YA UKUHANI -1 ITUMIE VYEMA NEEMA YA UKUHANI -1 Reviewed by Unknown on 9:02:00 PM Rating: 5

No comments:

Sora Templates