MAMBO YANAYOWEZA KUKUFANYA KUSHINDWA KUFIKIA MWISHO WAKO MUNGU ALIOKUPANGIA-1
LENGO KUU LA SOMO
Lengo kuu la somo hili ni kujitathimini uhusiano
wako na Mungu katika maendeleo yako ya kiroho, kibinafsi na kimwili katika
kufikia mwisho ambao Mungu amepanga ufikie katika kipindi chote cha maisha yako
hapa duniani.
Neno la Somo
Kumb 34:1-5
“1Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu
mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. BWANA akamwonyesha
nchi yote Gileadi hata Dani; 2 na Naftali yote, na nchi ya Efraimu
na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi; 3 na
Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari. 4
BWANA akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo,
nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini
hutavuka huko. 5 Basi Musa, mtumishi wa BWANA, akafa huko, katika
nchi ya Moabu, kwa neno la BWANA.”
Kuna vitu ambavyo vinakufanya usiweze kufikia mahali
Mungu alipotaka ufike ama usiweze kupata vitu ambavyo Mungu alitaka upate. Japo
kwa macho ya damu na nyama tunaona kuwa ni vitu vidogo na vya kawaida sana
lakini vinaathari kubwa sana katika ulimwengu wa roho katika mahusiano ya mtu
na Mungu.
Sehemu ya Kwanza
HASIRA
NA KUTOKUAMINI (UTII)
Maandiko yanasema katika Kumb 34 kuwa Musa alikufa
huko katika nchi ya Moabu katika kilele cha Pisga katika mlima Nebo kwa NENO LA
BWANA.
Ukisoma vizuri kitabu cha KUMBUKUMBU utagundua kuwa
Mungu hakutaka Musa aishie Moabu bali alikusudia afike nchi ya ahadi yaani
Kaanani. Maandiko yanasema kuwa Musa alikufa akiwa na miaka 120, jicho lake
halikupofuka wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.
Mungu alimpa Musa kazi kubwa mbili;
(1) Kuwatoa wana wa Israeli kutoka mikononi mwa
Farao katika nchi ya Misri ambapo walikaa kama watumwa kwa zaidi ya miaka 400. Kutoka 3:10 inasema “Haya,
basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa
Israeli, katika Misri.”
(2)
Kuhakikisha kuwa wana wa Israeli wanafika Kaanani.
Kutoka 3:9,17“Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikia; tena nimeyaona
hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka
katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkaanani, na Mhiti, na
Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.”
Lengo la Mungu lilikuwa Musa na Haruni waingie
Kaanani pamoja na wana wa Israeli wote, lakini hawakuweza kuingia kwa sababu ya
kuasi (kwenda kinyume cha neno la Mungu) walipo upiga mwamba ili utoe maji
badala ya kuuambia kama BWANA alivyokuwa amewaagiza.
Hesabu 20: 7-13“7 BWANA akasema na Musa, akinena, 8...ukauambie
mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake…..11 Musa akainua mkono
wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi,
mkutano wakanywa na wanyama wao pia. 12 BWANA akamwambia Musa na
Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana
wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko katika ile nchi
niliyowapa. 13 Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa
Israeli waliteta na BWANA, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.”
Shida iliyokuwa ikimsumbua Musa ni hasira. Tangia
Musa anaitwa na Mungu alikuwa akifanikiwa kutengeneza mambo yake na ya watu
wake kila wanapokosea lakini safari hii hakufanya hivyo ikapelekea kifo chake
na cha ndugu yake Haruni na hapo ndipo ilipo kuwa mwisho wa safari yao (Musa na
Haruni) kuelekea Kaanani. Kifo cha Haruni (Hesabu 20:22-29), kifo cha Musa
(Kumb 32:48-52; 34:1-5).
Lakini katikati ya safari kutoka Misri kwenda
Kaanani liliibuka swala la kuandika Torati (Kumb 31:24 “Basi ikawa hapo Musa alipomaliza
kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha,”).
Musa na Haruni hawakumwamini na hawakumtakasa Mungu
katika maji ya Meriba huko Kadeshi kwa kuupiga mwamba badala ya kuuambia utoe
maji kama Mungu alivyo waagiza wafanye.
Mbali na kutokuamini kwao, lakini kitu kingine ni
kuwa Musa alikuwa hapendi sana kuona wana wa Israeli wanalalamika lalamika juu
ya Mungu ama wakienda kinyume na mapenzi ya Mungu. Hivyo, wakati mwingine
walipo kuwa wakimlalamika au walipokwenda kinyume, Musa alikasirika sana na
yeye analalamika kwa Mungu. Hesabu 11:4-15 “10Basi Musa akawasikia watu
wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za
BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika. 11 Musa
akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata
neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? 12Je!
Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote...”
Kutoka 32:19 “Hata alipoyakaribia marago akaiona ile
ndama, na ile michezo.Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi
mwake, akazivunja chini ya mlima.”
Ukisoma Hesabu 20 utakuja kuona kuwa kitu ambacho
wana wa Israeli walikifanya katika sura ya 11 ndicho hicho pia wanakifanya sura
ya 20. Walikuwa ni watu wa kulalamika kila wanapo pungukiwa na jambo fulani
katika safari yao. Na macho yao yote yalikuwa ni kwa Musa. Ilifika wakati Musa
alichoshwa na lawama zao na kutokuridhika kwao hali iliyokuwa ikimfanya
akasirike sana hata kufikia kumwomba Mungu amuue “Na kama ukinitenda hivi,
nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami
nisiyaone haya mashaka yangu” Hesabu 11:15.
Hesabu 20:10 inatuonyesha dhahiri kuwa Musa alikuwa
amekasirika sana. Hii tunaiona ambavyo Musa aliwaita wana wa Israeli baada ya
kuwakusanya, aliwaita ‘waasi’. Musa
alisema “…Sikieni sasa, enyi waasi; je!Tuwatokezee maji katika mwamba huu?” Hilo
neno waasi
kwenye tafsiri ya kiingereza limetumika neno ‘rebels’ ambalo ni‘a
person who resists an established authority, often violently’. Maana
yake kwa Kiswahili twaweza sema ni ‘mtu anayepinga au anayezuia mamlaka
yaliyoanzishwa kwa njia ya machafuko’
Sasa Musa aliwaita watu wa Israeli rebels (waasi), watu wanaopinga mamlaka
yaliyopo. Hii inatuonyesha kuwa Musa alikuwa na ghadhabu juu yao kutokana na
neno alilolitumia. 1
Samweli 15:23 “Kwani kuasi ni
kama dhambi ya uchawi…”.1 Yohana 3:4 inatupa maana ya neno UASI, “Kila
atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.”
Tatizo la Musa kutokufika nchi ya ahadi halikuwa ni
hasira, bali ni matokeo ya hasira yake. Maandiko yanatuweka wazi kuhusiana na
hasira ya mpumbavu na hasira ya mchukia uovu (hasira takatifu). Maandiko
yanaposema hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu, haimaanishi kila mwenye hasira ni
mpumbavu bali inategemea ni aina gani ya hasira na inaleta matokeao gani.
Ayubu 5:2a; 36:18a inaposema “Kwani hasira humwua mtu
mpumbavu” “Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha;”
haimaanishi kila mwenye hasira atakufa ila inategemea ni aina gani ya hasira
mtu aliyokuwa nayo. Hasira inayomwua mtu mpumbavu ni hasira ya kutaka uovu au
hasira ya kuleta matokeao ya uovu. Pia hasira yaweza kuwa takatifu (hasira ya
kuchukia uovu) lakini mwisho wake ikakupeleka kutenda jambo lisilo takatifu
mbele za Mungu ndio maana maandiko yanasema basi ujitunze, isije hasira
ikakuvuta hata ukafanya mzaha.
Mungu na Musa
wote walipata hasira juu ya watu wa Israeli kwa kulalamika lalamika. Mungu
hapendi uovu. Ndio maana hukasirika pale mtu anapotenda uovu ila humpenda mtu
anaechukia uovu. Mungu alipenda jinsi ambavyo Musa anachukizwa na matendo maovu
ya watu wa Israeli kwa maana “Mshindo wake hutoa habari zake, Anayewaka hasira juu ya uovu” Ayubu 36:33.Ufunuo 2:2-6“2Nayajua matendo yako, na taabu yako, na
subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena
umewajaribu wale wajiitao mitume…3tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili
ya jina langu, wala hukuchoka.4Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha
upendo wako wa kwanza.5Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo,
naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.6Lakini unalo neno
hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.” Hebu soma kwa kuunganisha maneno yote niliyoyapigia
mstari hapo juu (Ufunuo 2:2-6) utapata kuona nini BWANA anachotaka uone
kilichotokea kwa Musa.
Tatizo
lililomkuta Musa ni matokeo ya hasira yake. Ayubu 36:18 “Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha;” Musa hasira yake ilimvuta kumpeleka upotevuni japo
alikuwa na hasira takatifu (yakuchukia uovu). Musa na Haruni walifanya kosa
kubwa moja ambalo ni ‘kutokumwamini
Mungu ili kumstahi mbele ya macho ya wana wa Isaraeli’ (Hesabu 20:12). Kosa
hilo moja limegawanyika katika sehemu mbili;
i.
Walijitwalia utukufu
ii.
Hawakutii agizo la Mungu
Kujitwalia Utukufu
Hesabu 20:10 “Musa na
Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi
waasi; je! Tuwatokezee maji
katika mwamba huu?”Hebu litazame kwa makini neno ‘tuwatokezee’ nililolipigia mstari. Musa na Haruni waliichukua
nafasi ya Mungu wakajiweka wao kana kwamba wao ndio wanaofanya maji yatoke
katika mwamba. Hawakumrudishia Mungu utukufu kwa jambo hilo. Walisema ‘tuwatokezee…’ (sisi), badala ya kusema ‘je! BWANA awatokezee…’Ni kweli kuwa
katika mstari wa 8 Mungu alimwambia Musa ‘…nawe
utawatokezea maji katika mwamba…’ lakini haikuwa sababu ya kumfanya Musa
ajitwalie utukukufu japo alipewa nafasi ya kuwa mungu kwa Haruni.
Jambo hili alilolifanya Musa ni tofauti na alichokifanya katika
kitabu cha Kutoka 14:13“Musa
akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia
leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele” ambapo
wakati Israeli wanaogopa jeshi la Farao na mbele yao kukiwa na bahari, Musa
aliwaambia wasiogope maana Bwana atawafanyia wokovu, hakusema msiogope maana
tutawafanyia wokovu. Kwa maana nyingine alitambua kuwa Mungu ndie atendae
kupitia yeye (Musa).
Kosa hilo la kutomrudishia Mungu
utukufu lilimpelekea kufa katika mlima Nebo kwenye kilele cha Pisga. Matendo
12:23 inatuonyesha wazi kuwa malaika wa Bwana alimpiga mfalme akafa hapo hapo
kwa kosa la kutomrudishia Mungu utukufu, “Mara malaika wa
Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa
na roho.”
Kutokutii agizo la
Mungu
Mungu alimwambia
Musa, wakusanye mkutano kisha wewe na Haruni ndugu yako ukauambie mwamba mbele
ya macho yao utoe maji yake (Hesabu 20:8). Musa na Haruni hawakulitii agizo la
Mungu maana badala ya kuuambia mwamba wao wakaupiga kwa fimbo, “Musa akainua mkono
wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili;” (Hesabu 20:11a).
Kumb 32:48-51 “48Bwana
akasema na Musa siku iyo hiyo, akamwambia,49Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho
katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana
wa Israeli kuimiliki;50ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa
zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe
pamoja na watu wake51kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati
ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa
kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli.”
Kumbukumbu la
Torati imetupa sababu ya na Haruni na Musa kufa, hii yote ni kwa sababu
walikosa kumtii Mungu mbele za wana wa Israeli. 1Samweli 15:22b inasema “Angalia, kutii ni
bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.”
Hatuwezi kumtukuza Mungu kwa namna iwayo yote na kufikia mwisho wetu mwema kama hatutakuwa na
utii ndani yetu.
Fuatilia mwendelezo wa somo hili.
MAMBO YANAYOWEZA KUKUFANYA KUSHINDWA KUFIKIA MWISHO WAKO MUNGU ALIOKUPANGIA-1
Reviewed by Unknown
on
12:45:00 PM
Rating:
Mungu akubariki na kujupa mafunuo mengi kwa neno zuri, amen!
ReplyDelete