BREAKING NEWS

[5]

NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU-4



KAZI NA NGUVU YA NEEMA
Karibu katika mwendelezo wa somo hili. Baada ya kuona namna neema inavyojifunua, ni vyema sasa kujifunza namna neema hiyo inavyotenda kazi na nguvu inayoachiliwa wakati wa dhiki. Kimsingi, namna neema inavyojifunua ina uhusiano mkubwa na namna hiyo neema inavyofanya kazi. Tunahitaji kujua msaada unaotokea kutoka katika neema ilyoachiliwa kwako wakati wa shida, vikwazo, magumu na dhiki.

Wakati tunaanza somo hili nilisema wazi kuwa, Mungu anajua mazingira halisi tuliyonayo huku duniani, lakini anahitaji tuishi maisha ya kumpendeza na ya ushindi. Kuna wakati tunazungukwa na mazingira ya dhambi, lakini katika mazngira hayo Mungu hategemei tumkosee. Biblia inaweka wazi kuwa, Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” Warumi 6:1-2. Ikiwa na maana kuwa sisi tulioifia dhambi kwa kuzaliwa mara ya pili hatupaswi kudumu katika dhambi tena. Hatupaswi kuishi katika dhambi. Dhambi ijapokusonga inakupasa uishinde.  Hili ndilo tegemeo la Mungu kwa mtu wake huku duniani. Neema inafanya yafuatayo:-


Kukupa ushindi juu ya dhambi
Neema ya Mungu ndiyo iliyotupa wokovu, na kwa neema hiyo hiyo tunalindwa tusiangukie dhambini. Neema ndiyo inayotusaidia tusiangukie dhambini. Ndiyo inayotusaidia kuendelea kusimama katika wokovu.

Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.” Warumi 5:1-2

Kwa neema ya Mungu tunaendelea kusimama katika wokovu, ndiyo inayotupo nguvu ya kupigana na kuishinda dhambi. Uwezo wa kuendelea ndani ya Kristo, hautoki kwetu wenyewe bali Mungu huachilia kupitia neema yake

Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” 1 Yohana 5:18

Uwezo wa mtu kushinda dhambi hautegemei tu kwa sababu amezaliwa na Mungu bali uwezo wa kujilinda. Aliyezaliwa na Mungu anapokuwa na uwezo wa kujilinda, shetani hawezi kumgusa, wala kutenda dhambi. Anaposhindwa kujilinda hata kama amezaliwa na Mungu, dhambi ataitenda. Kuzaliwa na Mungu ni mtaji wa kuweza kujilinda. Mungu hawezi kumwacha mtu aliyemzaa mara ya pili hivi hivi bila kumpa uwezo wa kujilinda. Uwezo huu wa kujinda unategemea neema iliyo juu yake.

Warumi inatuambia “ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake”, kwa hiyo kwa imani tunaifikia neema ambayo ndani yake tunasimama. Mtu anapookoka anatakiwa kuendelea ndani ya neema aliyoipokea ili kudumu katika wokovu alioupata. Namna pekee ya kushinda dhambi na majaribu ya shetani ni kuelendelea na kukua katika neema aliyoipokea, kwa kuishi maisha yapasayo neema hiyo.  Neema ni ngao ya kukulinda na uharibifu wa adui. As longer as you continue in the grace, that grace become your shield from distructions and sins. Kwa kadiri unavyokua, ndivyo na neema inavyoongezeka.

Wako watu wanaochukulia neema kama kitu cha mchezo, kwa madanganyo ya shetani wanajiambia, mazingira yamekuwa magumu sasa, wacha nifanye tu hili (dhambi) hata Mungu anajua nimeshindwa, nitatubu baadaye, neema ipo. Paulo natuambia katika warumi 6:1-2 na kutukataza tusifanye hivyo. Maana kama umeifia dhambi utaishije katika dhambi tena. Neema ya Mungu haijawekwa namna hiyo. Neema imewekwa ili kwamba itakapokuokoa na dhambi ikulinde utakapoendelea ndani yake. 

Kukupa ufahamu na maarifa.

Tulikwisha kuzungumza hili katika namna neema inavyojifunua, na ndivyo hasa inavyoweza kumsaidi mtu kushinda majaribu, dhambi na dhiki alizonazo. Kushinda katika mazingira uliyonayo kunategemea sana na ufahamu unaoupata kuhusiana na mazingira hayo. Ufahamu huu ndio unaoweza kuutumia kuvuka kwa ushindi. Ndiyo maana unapokuwa kwenye kipindi kigumu kunakuwa na vita kali sana juu ya kile unachokisikia. Shetani anatamani akusilizishe cha kwake na Mungu anatamani akusikilizishe neno lake na kukupa ufahamu wa kukusaidia kuvuka. Ndio maani ni muhimu kuwa makini juu ya kile unachosikia unapokuwa kwenye wakati mgumu.

Neema hutangulia kabla ya ufahamu na maarifa. Kimsingi neema ndiyo inayoachilia maarifa na ufahamu ndani ya mtu. Na neema huendelea kuongezeka kwa kadiri ya kuongezeka na kutumiwa kwa maarifa na ufahamu uliopokea.

“Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako” Kutoka 33:13

Musa alijua kanuni hii akamwomba Mungu, ikiwa nimepata neema, unionyeshe njia zako nipate kukujua. Musa alikuwa anaomba maarifa na ufahamu juu ya njia za Mungu ili amjue. Lakini alijua kuwa naweza kupata kupitia neema nitakayopata. Neema ilikuwa inafungua mlango kwa Musa kupata ufahamu na maarifa juu ya njia za Mungu. Kwa hiyo neema aliyoipata ndiyo iliachilia ufahamu na maarifa juu ya njia za Mungu. 

“Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.” Kutoka 33:17

Aliyoyaomba Musa yaliwezekana kwa sababu ya ile neema aliyopata. Lakini ona pia katika maombi ya Musa, anasema “….unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; …” Hii inatuonyesha kuwa, ufahamu na maarifa aliyoyakusudia yalilenga kuongeza na kupata neema zaidi kwa Mungu. Unapoona kuna maarifa yanaachiliwa kulingana na mazingira uliyonayo ujue neema ya Mungu ipo kazini.

Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” Tito 2:11-12

Tito inatuonyesha wazi kuwa, neema iliyofunuliwa juu ya mtu ina kazi ya kumfundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia. Ili kuishi kwa kiasi, haki na utauwa katika ulimwengu huu wa sasa unahitaji nguvu, ufahamu na maarifa ya namna ya kukataa ubaya na tamaa za kidunia. Neema ndiyo inayotoa darasa la namna ya kukataa ubaya na tamaa za kidunia. 

Unapokuwa hujui nini cha kufanya unapokuwa katika mazingira magumu, ni mbaya zaidi kuliko mazingira yenyewe. Unapokosa kujua cha kufanya, kunaondoa tumaini ndani yako na kujikuta huna mwelekeo wowote. Katika mazingira hayo, utakalofanya lolote ni sahihi kwako, ila matokeo ndiyo yatakayokuambia kuwa ni sahihi au la. Lakini ndani ya Kristo Mungu ameahidi kuwa hatutakuwa gizani, yaani kuwa bila ufahamu wa nini cha kufanya katika mazingira tutakayokuwa. Mungu huachilia neema itakupa ufahamu na maarifa ya namna ya kutoka salama. Neema inakuweka mahali ambapo unaweza ukaona mpenyo wa namna ya kuvuka. Inakupa nafasi ya kuona fursa ya namna ya kushinda.

Ona, Yusufu alipokuwa katika mazingira ya zinaa hatarishi, ufahamu pekee uliokuja ili kushinda ilikuwa ni kukimbia. Aliweza kuishinda ile tamaa ya kidunia, kwa fursa aliyoiona ya kukimbia. Kuna wakati unaweza ukawa unaiendea njia fulani, lakini gafla ndani yako unagundua njia uliyoiendea sio sahihi, huo ufahamu ndiyo umekuja ili kukuokoa na uangamivu wa njia uliyoichagua. Haleluya!!

Uwezo wa neema wa kuokoa

Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” Tito 2:11-12

Mungu anajua aina ya mazingira ya huku duniani kama nilivyotangulia kusema, ni mazingira magumu ambayo ukitaka kuishi maisha ya utauwa, ujiandae kwa dhiki. Kimsingi biblia imeweka wazi juu ya hili kwamba “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.” (2 Tim 3:12). Kwa hiyo ukitaka kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, kuudhiwa ni hakika. Hii ni kwa kuwa dunia iko kinyume chako, na utamaduni wako uko kinyume na wa kwake. Ni mambo yasiyo ya kwao. Dhuluma na matendo yasiyo haki yanapoendelea, yanamfanya mtu wa Mungu kuhuzunika rohoni, anapokuwa anaishi katikati yake. Mungu ni mwaminifu katika mazingira kama hayo, kwa watu wake. Aweza kukuokoa na kukupa ushindi. Biblia inasema:-

tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu;” 2 Petro 2:6-9

Lutu alijikuta kwenye mazingira magumu namna ya kuishi na Mungu wake. Akahuzunishwa sana na mwenendo mchafu na ufisadi wa watu aliokuwa anakaa katikati yao. Roho yake iliteseka siku baada ya siku, kwa uzinzi uliokuwa unafanyika Sodoma na Gomora. Kila siku ni afadhali ya jana. Biblia inasema kuwa Mungu alipoiendee hii miji kuangamiza, alimkumbuka Lutu akamwokoa. Katika mazngira hayo, Mungu anajua namna ya kuwaokoa watauwa wake. Inawezekana na wewe unayesoma mafundisho haya unapitia mazingira kama haya kazini, nyumbani kwako, katika ukoo wako, katika jamii yako, Mungu atakuokoa na mazingira hayo na kukupa ushindi mkubwa. Alimwokoa Lutu atakuokoa na wewe.

Nuhu alipata shida ile ile kama ya Lutu, na Mungu wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu”  2 Petro 2:5. Nuhu aliokolewa kama Lutu alivyookolewa.

Kilichowaokoa hasa hawa ndugu ni ile neema waliyoipokea toka kwa Mungu. Wasingepata neema na wao wangekuwa kama wengine. Kwa sababu neema ndiyo yenye nguvu ya kuokoa.

“Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana”  Mwanzo 6:8

Neema aliyoipata toka kwa Mungu ndiyo iliyomwokoa Nuhu pamoja na watoto wake, na sio safina iliyotengezwa. Kusingekuwa na neema juu yake, safina aliyoitengeneza ingeangamia pia. Maana kama Mungu aliangamiza dunia nzima aliyoifanya yeye mwenyewe, si zaidi sana safina ilitengenezwa na mikono ya Nuhu. Lakini neema juu yake iliendelea kushikilia mafuriko ya ghadhabu ya Mungu, ikalinda safina isiangamizwe pamoja na wengine. Neema ilifunuliwa kwake ikamwokoa Nuhu na watoto wake. Nuhu aliona fursa ya kuokolewa ndani ya neema aliyopata katika gharika iliyokuwa inakuja. Kilichowatofautisha Nuhu na wengine, ilikuwa ni uwezo wa kutumia neema vizuri. Aliamini alichoambiwa na akapata wokovu.

Uhusiano wa neema na imani katika kuokoa

Kuna uhusiano mkubwa kati ya neema na imani. Imani inafanya neema iliyo juu yako itende kazi ipasavyo. Uwezo wa neema wa kuokoa unategemea imani unayokuwa nayo.

Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;”  Efeso 2:8

Efeso inatufundisha kuwa neema ndiyo inayookoa ila inatumia imani kuokoa. Tito 2:11 inatuambia, neema ndiyo inayookoa wanadamu. Kumbuka imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17), na kazi mojawapo ya neema ni kukupa ufahamu na maarifa namna ya kuvuka katika mazingira uliyoayo. Kazi kubwa unayokuwa nayo ni kuamini ulichofunuliwa wakati huo. Unaposhindwa kuamini, neema inakuwa bure bila kazi. Nuhu aliposikia kwamba kuna gharika inakuja, na kwamba anatakiwa kujenga safina, akaamini na kujenga safina. Neema aliyopata ikafanya kazi yake ipasavyo. Wengine walisikia hawakutaka kuamini, hasara ikatokea kwao. Faith makes grace effective.

Shida kubwa ya sasa sio kwamba hakuna neema tunapokuwa katika mazingira magumu, bali kuamini tunachoambiwa na Mungu wakati huo. Na kwa kushindwa kuamini, biblia inatuambia kuwa tunakuwa tumeipokea bure neema yake. “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2 Wakorintho 6:1). Tunaposhindwa kuitumia neema ipasavyo, inakuwa tumeipokea bure au tumeipungukia neema hiyo.

Nguvu ya kustahimili

Mwaka 2012, nilihudhuria kongamano la vijana lililokuwa limekusanya vijana kutoka nchi zaidi ya sita barani Afrika na lilifanyikia Boko, Dar es Salaam. Kongamano lilihusu kujifunza neno la Mungu pamoja na maswala ya uongozi. Siku ya mwisho, baada ya kumaliza kongamano, vijana waliotoka nje ya Tanzania walitamani kuzunguka na kuuona mji. Wakati wa kuzunguka, tukiwa kwenye gari, nikawa nabadidilishana mawazo na dada mmoja kutoka Nigeria, na akawa ananipa stori ya mwenzake mmoja ambaye alikuwa amemaliza chuo na hakubahatika kupata kazi kwa mda mrefu. Katika kipindi hicho kirefu alikuwa anaendelea kumwomba Mungu afungue milango. Na hatimaye Mungu akamwambia mlango wako wa mafanikio haupo huko alikoomba bali akamwongozo kufanya biashara ndogo ya kuuza karanga, na baadaye ikawa kubwa, akafungua na biashara nyingine. Na sasa amekuwa mfanya biashara mkubwa ambaye hatumii alichosoma shule. Yule dada akaniambia, Mungu anaweza kukubadilishia mwelekeo kama anavyotaka. Nilipomsikiliza, nikamuuliza swali, uwezo wa kustahimili kipindi kirefu namna hiyo aliupata wapi? Na uwezo wa kuanza upya aliupata wapi? Ninawezaje kuanza upya namna hiyo? Akaniambia “aliomba neema ya Mungu juu yake na wewe utaomba hiyo neema”.
Aliponiambia hayo maneno, yalinifikirisha sana, nikajua ufahamu wake juu ya neema ya Mungu ni mkubwa kuliko mimi. Kimsingi somo hili lilizaliwa siku hiyo. Neema ilimsaidi yule ndugu kuvumilia na kustahimili ile dhiki ya bila kuwa na kitu. Hata Mungu alipompa kitu kingine cha kufanya bado alistahimili.

Nguvu ya kustahimili ni uwezo wa mtu wa kuweza kuvumilia. Uwezo huu tunajifunza kwa Mungu mwenyewe. Biblia inatuambia kuwa:

“ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa”  Warumi 3:25

Toka Adamu alipofanya dhambi mpaka ukombozi ulipotufika, hatukuangamizwa kwa sababu hizo dhambi ziliachiliwa kwenye ustahimili wa Mungu. Uwezo wa Mungu wa kustahimili ndiyo uliomfanya kutuvumilia katika dhambi zetu mpaka wakati mkamilifu wa wokovu. Vinginevyo tungekuwa tumefutiliwa mbali tayari. Kama Mungu anavyoweza kustahimili, ndivyo na sisi tunatakiwa kuwa na uwezo wa kustahimiri dhiki, na majaribu yanayotupata.

“Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele”  2 Tim 2:10

Paulo anasema anastahimili mambo yote kwa ajili ya wateule. Alikuwa na uwezo wa kuvumilia mapingano makuu aliyokuwa anapitia, na dhiki nyingi kwa ajili ya utumishi aliokuwa nao. Biblia inasema “ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake…” (Warumi 5:2). Paulo aliweza kustahimili dhiki kwa sababu ya neema aliyokuwa anatembea ndani yake, iliendelea kumuonyesha yaliyo mbele na kumtia nguvu ya kuvumilia. The grace of God, when is fully relied, become the power of endurance. Paulo alipobanwa na mwiba, Mungu alimwambia neema yangu yakutosha. Neema ilikuwa ndio kitu cha kumtia nguvu ya kuvumilia na kustahimili maumivu.

Kumbuka haijalishi mazingira uliyonayo, hakuna kitu cha kujitetea kama ukianguka. Biblia katika waebrania 12:15 inatushauri tusiipungukie neema ya Mungu, kwa kuacha mazingira kutushinda. Kuna mlango wa kutubu na kumrudia Mungu tunapojikuta mazingira yametushinda. Kwa mazingira tuliyonayo. Tunahitaji neema ya Mungu kuishi kwa ushindi. Yes we need the grace.

Barikiwa, tumefika mwisho wa somo hili. Usiache kutembelea blogu yetu kwa mafundisho zaidi.
NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU-4 NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU-4 Reviewed by Unknown on 12:20:00 AM Rating: 5

19 comments:

  1. Mungu ni mwema sana. Yaani hili somo limenibariki na kunivusha . Kuna mahali nimevuka kwa kujua somo hili. Ubarikiwe Mtumishi .

    ReplyDelete
  2. Somo ni zuri saaaana, ubarikiwe!

    ReplyDelete
  3. Mungu akubariki maana nimeelewa ukuu wa neema ya Mungu juu ya maisha yetu.

    ReplyDelete
  4. Yukon Casino - Casino in thakasino.com
    Get the best of the best online gaming experience at Yukon Casino with link 12bet all your favourite m88 slots, 10cric login table games and video poker games.

    ReplyDelete
  5. Ubarikiwe san Mtumishi wa MUNGU somo nzuri san

    ReplyDelete
  6. SoMo zuri mno barikiweni sana

    ReplyDelete
  7. Barikiwa Sana mtumishi umenisogeza mbele kiroho

    ReplyDelete
  8. Nakuomba Hilo Somo kwa wasap 0789510799

    ReplyDelete
  9. Barikiwa sana mtumishi, Mungu azidi kukufunika na neema yake katika ufahamu na ujuzi wa neno lake uendelee kutufundisha

    ReplyDelete
  10. Ubarikiwe sana mtumishi wa Mungu, somo ni zuri sana Sana. Natamani kujifunza zaidi kuanzia mwanzo wa somo. Please naomba ikikupendeza unitumie huku kwa whatsap yangu 0757530555

    ReplyDelete
  11. Nimebarikiwa sana ubarikiwe mtumishi

    ReplyDelete
  12. Mungu akupe mwisho mwema

    Bariki wa sanaaa

    ReplyDelete
  13. Mungu Akijaziye zaidi neema yake

    ReplyDelete
  14. Ubarikiwe Kwa Somo zari.

    ReplyDelete

Sora Templates