NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-7
NAMNA
YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO
Baada ya safari ndefu ya kujifunza, sasa ndio tunamalizia kipengele cha mwisho
USHIRIKA NA WAPENDWA/WATAKATIFU
Ukiwa
na ushirka na wapendwa wengine ni jambo muhimu sana katika kuhakikisha unakua
na kuimarika katika maisha ya kiroho. Katika ushirka na watakatifu au wapendwa
wengine kuna makundi matatu hivi. (a) watu wa jumuiya moja nikiwa na maana ya
kanisa au mwili wa kristo, (b) Marafiki, (c) Baba wa kiroho. Makundi haya
ukiyakosa, maisha ya kiroho yanakuwa magumu sana na kwa hiyo ukuaji kiroho
unakuwa wa taabu sana.
“Afadhali
kuwa wawili
kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao” Muhubiri
4:9
Hakuna mtu anayeweza kujijenga na
kujiimarishaa peke yake, ni lazima kuwa katika ushirika na wapendwa wengine,
maana ni afadhari kuwa wawili kuliko mmoja, maana watapata ijara njema kwa kazi
yao. Sentensi hii inamtazamo kwamba, kazi italeta matokeo mazuri zaidi kama
kutakuwa na ushirikiano wa watu wawili kuliko mmoja. Kushiriki na wengine
kunaleta ufanisi wa jambo na uharaka wa kufanikisha jambo. Jambo linaweza
kumchukua mtu mda mrefu kulifanikisha akiwa peke yake kuliko
akishirikiana na mwingine. Na mtu anapokuwa anashiriki mara kwa mara na watu
wengine kwenye maswala ya kiroho anakua haraka zaidi kuliko yeye anayekaa peke
yake mda wote.
“Tena, wawili
wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje
kuona moto?. Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki” (Muhubiri 4:11-12)
Katika safari ya kiroho sio njema
kutembea peke yako, unahitaji watu watakao kuwa pamoja na wewe kukutia moyo,
kukufariji, kukutia joto, kukufundisha, kukuonesha njia sahihi ya kupita, wa kuvipiga
vita pamoja na wa kukusaidia kubeba mizigo. Na Mungu hawezi kukuacha tu peke
yako, lazima atakuletea watu kuwa karibu nawe kwa makusudi. Na watu watakaokuja
watakuwa katika makundi hayo hapo matatu, na natamani kuelezea moja baada ya
lingine.
WATU
WA JUMUIYA MOJA AU KANISA
Kusanyiko la kanisa ni muhimu
sana kwa ukuaji wa kiroho wa mtu. Nazungumzia kanisa kama kusanyiko la watu
walizaliwa mara ya pili na wanaoliitia jina la BWANA kwa moyo safi, Huko
unajifunza na wewe namna ya kuliitia jina la BWANA kama wao.
“Wala tusiache kukusanyika pamoja, Kama ilivyo desturi ya wengine; Bali
tuonyane; Na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa
inakaribia” (Waebrania
10:25)
Biblia inatoa maagizo kwamba tusiache
kukusanyika kama ilivyodesturi, kwa maana huko tutaweza kuonyana, na kutiana
moyo wakati tunamsubiri Yesu kuja mara ya pili. Kwa kadiri jinsi siku ile
inavyokaribia, tunashauriwa kukusanyika pamoja na kuonyana. Neno ‘bali’
linatupa kuona kwamba, tunapaswa kukusanyika zaidi ya desturi yaani kwa lengo
maalumu ikiwa ni pamoja na kuonyana. Tunapojumuika na wengine huko tunajifunza
namna wengine wanavyofanya, namna wanavyomtafuta BWANA.
Kanisa ni mwili wa Kristo. Penye kusanyiko
ambapo ni mwili wa Kristo, ndiyo mahali sahihi kukusanyika. Ukusanyikapo sehemu
kama hiyo, unaenda kama mmojawapo wa kiungo katika huo mwili. Utendaji kazi wa
kiungo kimoja unategemea sana viungo vingine katika mwili. Kwa maneno mengine
inaweza kusemwa kwamba, udhihirisho wa kiungo kimoja, unategemea kiungo
kingine, na kazi yake inakuwa na matunda kwa msaada wa kiungo kingine katika
mwili mmoja. Kwa mfano, ili mikono iweze kufanya kazi kubeba na kuhamisha kitu,
inahitaji macho yanayoweza kuona sawa sawa kitu chenyewe na miguu ya kumpeleka
mahali kitu kilipo. Kazi ya mikono itakuwa ina matunda kama msaada wa miguu na
macho utakuwepo kupeleka hicho kitu kinapotakiwa. Kazi ya mikono inakuwa
malidhawa kwa sababu ya msaada wa viungo vingine katika mwili. Ndivyo hivyo
hata katika mwili wa Kristo, mtu hawezi kujiimalisha peke yake bila kujumuika
na kupata msaada wa wengine. Inapaswa kujumuika sio tu kama desturi bali kwa
sababu ni muhimu.
“Maana kama vile mwili
ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi,
ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote
tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa
tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili
si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si
wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si
jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa
jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia
viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka”
1 Wakorintho 12:12-18
Wako watu
wanaosema kwamba sio muhimu kukusanyika pamoja kwa sababu hata nyumbani Mungu
anamsikia akiomba. Hii ni ishara ya kutawaliwa na roho nyingine isiyo ya Kristo
Yesu. Maana sisi kwa Roho mmoja tulibatizwa KUWA MWILI MMOJA. Roho wa Mungu
tuliyempokea ndiye aliyetufanya kuwa mwili mmoja, na hauwezi kujitawanya alafu
ukabaki salama. Kiungo kimoja kinapokosekana katika mwili, mwili unaitwa
mlemavu, na wala kiungo hakiwezi kuwa na uhai tena na kufanya kazi
iliyokusudiwa. Kiungo kinaitwa ‘waste’ kwa sababu kinakuwa hakina kazi tena kwa
sababu uhai wake unategemea uhai wa mwili kwa roho iliyo ndani ya mwili. Kwa
hiyo inatupasa kukusanyika kwa kuwa sisi tu sehemu ya mwili mmoja, kuimarika
kwetu kunategemea kusanyiko hilo.
Sababu nyingine
inayotufanya tukusanyike ni kwamba kila mtu amepewa kipawa chake. Hiki kipawa kinatumika
katikati ya kusanyiko, na ili kukifaidi ni lazima uwe sehemu ya kusanyiko.
“Naye aliyeshuka ndiye
yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa
wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na
wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata
kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote
tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu
mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe
tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa
elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu” Waefeso 4:10-14
Mungu aliamua kuweka
vipawa mbalimbali ndani ya mwili wa kanisa, akijua kabisa ujumla wa vipawa
hivyo ndiyo unaoweza kuwaimarisha watakatifu wake. Aliwafanya wengine kuwa
mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu kwa kusudi la:- a)
Kuwakamilisha watakatifu, b) Kazi ya huduma itendeke, c) kuujenga mwili wa
kristo. Kwa hiyo kukamilishwa kwa mtu na kujengwa kwa mwili wa Kristo
kunategemea vipawa vya watu wengine ndani ya kanisa (mwili wa kristo). Na hapa
iko wazi kwamba hivyo vipawa vitaendelea kufanya kazi hata tutakapoufikia umoja
wa imani, kumfahamu sana mwana wa Mungu na kuwa mtu mkamirifu kwenye cheo cha
utimilifu wa Kristo. Ni wazi kwamba mtu hataweza kufikia ukamilifu katika kiimo
cha utimilifu wa Kristo, bila vipawa hivi walivyonavyo watu wengine ndani ya
kanisa. Kwa hiyo kuwa kwenye kusanyiko la kanisa sio chaguo (optional), ni kitu
cha lazima kama unataka kukua na kuimalika. Hata kama unajitahidi sana kusoma
biblia kuna mambo huwezi elewa peke yako, kuomba sana, kuna mambo huwezi yapata
ukiwa peke yako. Biblia inasema “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu
watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba
yangu aliye mbinguni” (Math 18:19), kuna mambo ambayo Mungu hayafanyi isipokuwa
imepatana kuanzia wawili.
Natamani ujue ili kwamba “Lakini kila mmoja hupewa
ufunuo wa Roho kwa kufaidiana” (1 Wakor 12:7). Mungu akimpa mtu kipawa au
ufunuo sio kwa ajili yake bali kwa ajili ya kuwafaidia wengine. Kama Mungu
amekufanya mchungaji au mwalimu, sio kwa ajili yako bali kwa ajili ya
kuwafaidia wengine. Ukweli huu utakufanya utafaute watu wengine ambao utakukuwa
unawachunga na kuwafundisha, kwa sababu kipawa chako kitaendelea kukua na
kuimarika kwa kadiri unavyoendelea kukitumia. Unapojua kuwa vipawa vilivyo
ndani ya kanisa sio kwa ajili ya hao walionavyo bali kuwafaidia wengine ndani
ya kanisa ikiwa ni pamoja na wewe kama ukiwa ndani yake, itakufanya ufanye
bidii kukusanyika ili kuweza kuvifaidi. Kimsingi ndio maana hatutakiwi kuoneana
wivu kwa sababu ya hizi karama na
vipawa, kwa sababu walionavyo wamepewa kwa ajili ya wale wasionavyo na sio kwa
ajili yao. Mwalimu amewekwa na Mungu ili wewe ujifunze siri za Mungu, kumwonea
wivu na kumchukia ni kumwambia Mungu sitaki kujifunza neno lako.La hakika ni
kwamba, yale yote ambayo Mungu huyaweza ndani ya kusanyiko, mtu hawezi kuyapata
kama haudhurii kwenye hilo kusanyiko.
Muhimu kukumbuka
kwamba, Sio kila sehemu ni mahali sahihi kukusanyika. Kama nilivyotangulia
kusema, kusanyiko unalojuika nalo ndilo lenye nguvu ya kukuimarisha kiroho kwa
sababu ya mambo yanayotukia huko. Lakini pia kusanyiko lina nguvu ya kukubomoa
na kukuangamiza. Kwa hiyo ni muhimu kuangalia aina sahihi ya kusanyiko
unalotaka kujumuika nalo. Kwa sababu mambo yanayofanyika hapo ndiyo
yatakayosukuma mwelekeo wa maisha yako.
“Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko
la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu” Zaburi 22:16
Daudi aliona
kusanyiko la waovu limemzingira, na kazi yao kubwa ilikuwa ni kumfunga mikono
na miguu yake asiweze kupiga hatua na kufanya kazi impasayo. Kuna mahali
pengine ukienda kukusanyika, yaani ndiyo unadidimia kabisa kwa sababu ya aina
ya mambo yanayofanyika hapo mahali.Muhimu kuwa mahali ambao unajua utakula,
kunywa na kufaidi kazi za wengine.
MARAFIKI
Kabla ya kuona mchango wa rafiki kwenye
kuimarisha roho ya mtu na maisha ya kiroho, ni muhimu tukaelewa kwa nini maana
ya rafiki kiblia. Yesu aliwahi kusema maneno ambayo yanatupa kuelewa kwa undani
jambo hili,
“Hakuna aliye na
upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui
atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia
kwa Baba yangu nimewaarifu” Yohana 15:13-15
Kutoka katika maneno
haya tunaweza tukaona vinavyomfanya mtu kuitwa rafiki:-
Upendo
Ni lazima kuwepo na
upendo kati ya marafiki, na huo upendo unatakiwa ule wa kiwango cha juu, kuutoa
uhai kwa ajili ya rafiki. Yesu anasema hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu alafu anautaja kwamba wa
mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki yake, kwa hiyo kwa mtu kuutoa uhai
wake ndiyo kiwango cha mwisho cha upendo. Hii ina maana kwamba rafiki
wanatakiwa kupendana kwa maisha yao. Kulindana kwa maisha yao. Hii tunaiona
kwenye urafiki wa Yonathani na Daudi. Yonathani alimpenda Daudi kuliko nafsi
yake, yaani alikuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya Daudi kwa sababu uhai
wa rafikiye ulikuwa na thamani kuliko wake. Yonathani ndiye alikuwa mrithi wa
kiti cha kifalme baada ya baba yake Sauli, lakini kwa sababu ya rafiki yake
Daudi aliamua kuachana na nafasi na heshima. Kilichomfanya kuahirisha maisha
hayo ya juu na heshima katika nchi ni upendo aliokuwa nao kwa Daudi rafiki
yake. Alikuwa tayari kumtetea kwa baba yake na kuhatarisha maisha yake kwa
ajili ya rafiki yake.
Lugha moja
Rafiki ni yule ambaye
mnaongea lugha moja. Lugha moja ndiyo inayofanya kutembea njia moja na kutenda
kitu kimoja. Rafiki ni yule ambaye unaelewana katika usemi na matendo. Yesu
anasema mkitenda niwaamuruyo, mmekuwa rafiki zangu. Kutenda amuruyo ni kwa
sababu tumekubaliana naye. Anayeweza kukubaliana na wewe na kufanya
utakalokuifanya, kwa kukuunga mkono, ndiye rafiki. Haiwezekani mtu akawa rakini
lakini hampata katika maneno, mnayokubaliana hamtendi kwa pamoja. Biblia
inasema “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?”
(Amosi 3:3) kutembea pamoja ni matokeo kupatana. Kufanya kile Yesu
alichokiagiza, ndicho kinadhihirisha urafiki wetu.
Kujua siri
Yesu amesema wazi katika mistari
hii kwa nini hatuiti watumwa bali rafiki kwa sababu tumeshajariwa kuzijua siri
za Bwana wetu. Rafiki ni yule ambaye unaweza kumshirikisha na kumwambia siri
zako na yeye akakwambia zake. Ni yule ambaye yeye yuko wazi kwako na wewe wazi
kwake. Kwa sababu huwezi kumfunulia siri zako kila mtu, basi huyo rafiki
anatakiwa kuwa mtu mwaminifu mwenye kicho cha Mungu na msiri wa siri za Mungu
na rafiki yake. Ambaye hawezi kutoa nje siri za mwenzake la sivyo hakidhi
kigezo cha kuwa rafiki. Taarifa za ndani zinatakiwa zitoke kwa ruhusa ya wote
wawili. Ndio maana Mungu hafunui siri zake kwa kila mtu bali kwa wale
anaowaamini, rafiki zake ambao ndio wanaomcha. Biblia inasema “Mtu
na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu” (1 wakorintho 4:1). Mtu
ambaye unamshirikisha siri zako, inamaana unamshirikisha maisha yako. Kuna
wakati ambao unaweza ukawa unapitia changamoto za maisha, na hukutaka watu
wengi wajue lakini unahitaji msaada katika ilo, unatakiwa kuwa na rafiki
utakayemshirikisha hilo jambo na kusimama na wewe. Kuna wakati unahitaji mtu
ambaye atakuelewa vizuri katika mazingira unayopitia na kukusaidia kuvuka
vizuri. Na huyo anatakiwa kuwa rafiki. Huchukui tu kila mtu na kumwuita rafiki.
Rafiki lazima umpime na kurithika naye kabla hujawa karibu naye.
Katika
mambo haya matatu, tunaona wazi sawa na biblia inavyosema kwamba “…..rafiki
yako aliye kama moyo wako…” (Kumb 13:6). Anakupenda kwa maisha yake, kutunza na
kukusaidi kwenye madhaifu yako, kutunza siri zako na kwenda njia moja (kupatana
na kuelewana). Rafiki ni kama maisha yako. Kutokana na ukweli huu, ni muhimu
kuchagua rafiki ambaye atakuwa na tabia unazotaka, na mwelekeo unaotazamia
kuuendea. Kwa sababu mwelekeo anaouendea uwezekano ni mkubwa ukauendea huo.
Biblia inasema “Enenda pamoja na wenye hekima,
nawe utakuwa na hekima;
Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” (Mithali 13:20), kwa hiyo ni muhimu kujua
aina ya rafiki unayetaka, mpumbavu au mwenye hekima.
“Lakini
zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja
na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi”.
2 Timotheo 2:22
Unapotaka
kuimarika kiroho, ni muhimu ukachagua rafiki wa kuambatana naye ambaye anamwita
Bwana kwa moyo safi. Tumeitwa katika utakatifu ili tuingie katika
ushirika wa mwana wa Mungu. Tunatakiwa kuishi maisha yaliyotengwa na kuwa mbali
na tamaa za ujanani (dunia). Ili kuwa salama na kuhakikisha mbegu iliyo ndani
yako ya utakatifu inakuwa bila haiharibiwa , ni vyema kuwa na watu ambao
wanakuwa na aina ya maisha au ambao wanaishi kama wewe- wanaokataa tamaa za
ujanani (dunia) na kumwita Mungu kwa moyo safi. Mtu ili aimarike kiroho
anahitaji rafiki ambaye anamwita Bwana katika usafi wa moyo, kwa sababu naye
ndani yake atakuwa na hali ya kukataa dhambi, lakini pia lugha zenu zinakuwa
zinafanana. Mungu anaruhusu rafiki wa namna hii ili akuimarishe kiroho
katikakutengeneza tabia za kimungu.
Mara
unapookoka, alafu ukajitenga bila kushirikiana na wale waliokoka, ni rahisi
sana kwa sababu hutaweza kusimama peke yako. Unahitaji mtu atakayekufundisha
neno kwa karibu, mtu ambaye mtajumuika naye kwenye maombi mara kwa mara. Maandiko
yanasema katika Mithali 27:17:-
“Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake”
Kama vile chuma unavyoweza kunoa chuma, ndivyo ambavyo Mungu
kaweka marafiki ili kunoa rafiki zao, kuwaimarisha, kuwajenga rafiki zao
kuhakikisha kwamba nao wanakuwa imara kama wao. Marafiki kwa jinsi hii ni nzuri
sana, kwa sababu katika safari yenu kuna mambo ambayo Mungu atayafunua kwako na
kukufundisha lakini sio kwa rafiki yako wakati huo huo rafiki yako naye
anafunuliwa mengine na kufundishwa. Kwa kushirikiana, uliyofundishwa wewe na
rafiki yako, yanawajenga kwa pamoja. Mambo ambayo yangekugharimu muda mrefu
kuyafahamu, mnafanikiwa kuyajua kwa mda mfupi. Ndio maana napenda kuwa karibu
na rafiki zangu, tunalishana tu neno la Mungu kwa wengi.
Kama nilivyotangulia kusema hapo juu kwamba rafiki ni yule
anayekupenda kwa uhai wake (maisha), kwa sababu rafiki anatakiwa kudhihirisha
kiwango cha juu kabisa cha upendo. Rafiki wa aina hii hahesabu mabaya wala
makosa yako ufanyapo, anaweza kuchukuliana na wewe katika udhaifu ulionao, na
kutafuta namna ya kukusaidia ili kutoka katika makosa hayo na kutokurudia
makosa yale yale. Unahitaji rafiki ambaye atakuelewa na kukusaidia katika
makosa uliyofanya ambayo kwa kweli kila mtu asingitamani kuwa karibu na wewe
kwa sababu wamepoteza tumaini nawe kabisa katika wokovu wako.
Nina rafiki yangu ambaye katika safari tuliyonayo ya wokovu,
aliteleza na kuanguka katika dhambi. Watu wengine hawakutaka kuwa karibu naye
tena, walimwona mkosaji sana kuliko wao, imani yao juu yake ikapotea, naye
akajua hapa ndio basi pamoja na utumishi wake, na kuachana na wokovu. Kama
rafiki ikabidi nikae na kuzungumza naye, na kumweleza upendo wa Yesu. Kuanguka
sio mwisho wa safari ila ukiamua unaweza ukaufanya mwisho wa safari. Niamsaidia
namna ya kurudi kwa Mungu tena kwa toba na kuendelea na safariya wokovu.
Haleluya! Mungu yuko tayari kusamehe ila tu usirudie makosa yale yale.
Wengi wamepotea kabisa kwa kukosa marafiki wa kuwaelewa
katika hali zao na wakuwasaidia kurudi kwa Mungu na kuendelea na safari.
“Kwake huyo
atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye
kumcha Mwenyezi” Ayubu 6:14
Sijui kama unaona, Mungu anakupa
marafiki ili, wakati roho yako inataka au ndiyo inazimia, akutendee mema na kukurudisha
tena tena kwenye hali yako ya mwanzo. Anakupa ili kwamba utakapo kumwacha
Mungu, akutendee mema yaani kukurudisha tena. Ayubu kilimsumbua sana,
alitegemea hayo toka kwa rafiki zake walipokuja kumtembelea alipokuwa katika
magonjwa na adha, na shida nyingi, lakini rafiki zake walimkandamiza zaidi na
kumwona mkosaji. Ndivyo wapendwa wengi walivyo, badala ya kumsaidia kumsimaisha
mtu aangukapo, ndio wanamkakandamiza na kumtenga kabisa. Tuwapende hao na
kuwasaidia. Hii ndio maana ya kuwa rafiki.
BABA WA KIROHO
Katika mbio za wokovu ni muhimu
kuwa na baba wa kiroho, baba wa kiroho simaanishi tu yule ambaye alikuhubiria
ukaoka, bali pia yule ambaye anatakiwa kuwa pamoja na wewe kuhakikisha unakua
katika neema ya kristo na katika Kujua Mungu. Baba wakiroho simaanishi tu
wanaume bali na mwanamke pia.
Kuwa na baba wa kiroho ni muhimu
sana katika maisha. Yeye ndiye mwenye kwa kiasi kikuwa amekutangulia hatua
kadhaa, kule unakoelekea yeye alishapita tayari. Kuwa naye, anakupa na
kukuonyesha njia sahihi ya kuiendea, kukupa mwanga unapokuwa katika giza, kujibu
maswali yako yanayokutatiza.
Kazi kubwa ya baba ya kiroho ni
kuhakisha anaacha ndani ya mtoto alama yake, ili mtoto awe kama yeye. Anakazi
ya kutengeneza tabia ndani ya mtoto zitakazomsaidia kuishi ipasavyo hata kama
baba yake hayupo. Hii ndiyo kazi kubwa aliyokuwa nayo Yesu kwa wanafunzi wake,
alikuwa baba wa kiroho kwao (a mentor), kuwafundisha wanafunzi wake, kujenga
imani ndani yao, kuwapa nuru walipokuwa gizani, kuwaonesha njia sahihi ya
kuiendeana kufanya mambo, kujibu maswali waliyokuwa nao.
“basi, wakati huo
Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa Akamwendea Eli kwa haraka,
akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye
akaenda, akalala tena. Bwana akaita mara
ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa
maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa
hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana
akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi
hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita
yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa,
akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli
akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama
kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi
wako anasikia. Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika
Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha” (1 Samweli 3:4-11)
Baba wa kiroho ndiye anayeweza
kumsaidia mtu kuelewa kufanya vizuri kile asichokijua. Samweli alikuwa hajaijua
sauti ya BWANA bado, na kama angekuwa peke yake siku ile au bila baba wa
kumlea, kulikuwa na uwezekano mkubwa kutokuielewa na kushindwa kuitambua sauti
ya Mungu. Lakini Eli kwa kuwa yeye amekuwa katika utumishi, alielewa sauti iliyokuwa
na inamuita Samweli akamsaidia.
Kwa kuwa baba wa kiroho amekuwa
hatua nyingi mbele yako, anakuwa na wewe kukuleta kuyashiriki mambo mageni
ambayo hujawahi kuyapitia na kuonja kule ambako bado hujafika. Hili tunajifunza
pia kwa Yesu alipowachukua baadhi ya wanafunzi wake na kuwaleta katika mlima wa
mabadiliko (Mathayo `17:1-9), ili kwamba waweze kuuona na kuushiri utukufu ule.
Wako watu wanaosema wao
hawahitaji baba wa kiroho (a mentor), lakini Mungu amewaweka hao katikati yetu,
ili tuweze kuwafaidi. Makosa ambayo wao waliyafanya tusiyafanye sisi. Hakuna
haja ya kupasua miamba wakati wengine walishapasua kwa ajili yako. Kama unaye
usimwache akaenda zake, kama hauna muombe Mungu akupe mmoja.
Kuanzia mwanzo, tumekuwa
tukijifunza namna ya kukuza na kuimarisho roho yako, na nimejaribu kuelezea
mambo makuu manne ya msingi katika kuimarisha roho yako, nayo ni neno la Mungu,
kusifu na kuabudu, maombi na ushirika na watakatifu. Mambo haya ukiyazingatia na kuyaweka katika
matendo kwa uaminifu, utakuwa na kuimarika kwa kasi sana.
MWISHO
NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-7
Reviewed by Unknown
on
12:00:00 AM
Rating:
No comments: