NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO- 6
Tunaendelea na mwendelezo wetu, juu ya namna ya kukuza na kuimarisha roho yako. Karibu tuendelee.
Mambo haya waliyokuwa wanayafanya
akina Musa yalikuwa ni kivuli cha mambo yatakayokuja baadaye (wakati huu wa
sasa). Ingawa Mungu kwa rehema zake, alikuwa akijidhihirisha kwa Israeli pale
hema ya kwanza ilipokuwa ikisima, lakini njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa
haijadhihirishwa bado. Waebrania inatuambia;-
“Roho
mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa
bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama, ambayo ndiyo mfano wa
wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa
jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye” Waebrania 9:8-9
Patakatifu panapotajwa kwenye hii
waebrania ni tofauti na ile iliyokuwa kwenye hema ya kukutania wakati wa akina
Musa. Kwenye hii waebrania inapataja patakatifu pa mbinguni kabisa, ile ya
akina Musa ilikuwa kwa jinsi ya mwili. Ilikuwa sio halisi bali kivuli cha ile
ya mbinguni. Na maadamu ile ilikuwa bado inasimama, basi hii nyingine ilikuwa
bado kudhihirishwa. Njia ya kupaendea patakatifu kabisa pa mbinguni ilikuwa
bado haijadhihirishwa. Ile kusema njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa bado
haijadhihirishwa ina maana watu walikuwa hawana uwezo wa kupaingia patakatifu
(access to the Holy place). Patakatifu palikuwepo lakini watu walikuwa hawana
uwezo wa kupaingia.
Hapo patakatifu pa patakatifu pa
mbinguni, palipo na madhababu na kiti cha rehema, ndipo Mungu alipoweka nafasi
yetu ya kuwepo hapo kwa ajili ya kutoa ibada na maombi. Lakini mwanadamu hakuwa
na uwezo huo wa kusogea hapo, biblia inasema kwa sababu ya “dhambi” na kwa
sababu dhabihu na sadaka zilizotolewa hazikuweza kushughurikia hiyo dhambi na
kumkamilisha aabuduye. Dhambi ndiyo iliyokuwa kiambaza, na hii ilikuwa
inawakilishwa na ile pazia iliyotenganisha patakatifu na Patakatifu Pa
Patakatifu pale hema ya kwanza iliposimama.
Kuhani mkuu alikuwa akiingia
mahali patakatifu kutoa dhabihu na sadaka tena mara moja kwa mwaka kwa sababu
ya kumbukumbu la dhambi, hakuweza kuwafungulia wengine waingie mahali
patakatifu. Kuhani mkuu mwenyewe alipata nafasi ya kupaingia mahali patakatifu
kwa sababu ya ile sadaka ya dhambi ya kila mwaka. Dhambi (pazia) ilijenga
kiambaza na kuwazuia watu kuingia mahali patakatifu pale hema ya kwanza ilipokuwa
ikisimama, dhambi ndiyo iliyozuia kupaingia mahali patakatifu pa mbinguni
pasipotengenezwa kwa mikono ya wanadamu ingawa hapo ndipo Mungu anapotuhitaji
tuonekane.
Ili kuingia patakatifu pa
patakatifu mbinguni ilihitajika sadaka ambayo ingeweza kushughuria dhambi na
kutufungulia mlango kupaingia hapo na ilihitajika kuhani mkuu kufanya hiyo
sadaka.
“Kristo
alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia
kwenye hema iliyo kuu zaidi Na bora zaidi, ambayo haikujengwa Kwa mikono ya
binadamu, hii Ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. Hakuingia Kwa njia ya
damu ya mbuzi Na ya ndama, lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja
tu Kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele.” Waebrania 9:11-12
Haruni kama kuhani mkuu alikuwa
akiingia mahali patakatifu palipotengezwa na mikono ya wadamu akiwa na sadaka
na dhabihu za mbuzi na mafahali ambazo hata hivyo hazikuweza kumkamirisha yeye
aabuduye na kumleta karibu na Mungu lakinii Yesu kama kuhani mkuu aliingia
mahali patakatifu mara moja tu, sio kwa damu ya mbuzi na ya ndama bali kwa damu
yake mwenyewe. Biblia inaongeza kuwa aliingia mahali patakatifu akiisha kufanya
ukombozi wa milele. Hii inatupa kuona kwamba sadaka ya Yesu ilikuwa na kusudi
la kushughurikia kile kilichokuwa kiambaza cha kuingia mahali patakatifu.
Sadaka ya akina Haruni iliweza kutakasa watu kwa jinsi ya mwili, kwa hiyo
ilihitajika sadaka ambayo inaweza kushughurika roho na dhamiri za watu ili sasa
waweze kutoa ibada katika mahali patakatifu pa mbinguni kwa sababu tunapafikia
hapo kwa roho zetu.
“Basi
si zaidi sana damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi Yake kwa
Mungu kuwa sadaka isiyo na waa kutusafisha dhamiri zetu, kutokana na matendo
yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!” Waebrania 9:14
Damu ile ambayo Yesu aliingia
nayo mahali patakatifu ilikuwa na lengo la kushughuria roho na dhamiri zetu kuzitakasa
ili tuweze kupaingia mahali patakatifu kumwabudu Mungu aliye hai. Damu
inatuweka tayari kutoa ibada kwa Mungu. Ndiyo maana ilimpasa kabla ya kuingia
katika madhabahu ya mbinguni ilipasa kufanya ukombozi wa watu ili yeye atoapo
dhabihu ya damu yake wale aliowakomboa wawe na nafasi ya kupaingia mahali
patakatifu kama yeye. Kwa sababu dhambi ndiyo ilikuwa kiambaza, ilimpasa
ukifunje hicho kiambaza ili wale aliowakomboa waweze kuingia mahali patakatifu.
Biblia inasema alikivunja hicho kiambaza kwa “mwili” wake (Waefeso 2:15). Mwili
wake uliotolewa msalabani ulikwa kwa ajili ya kushughuria dhambi iliyotutenga
sisi na Mungu, iliyofanya uadui na kutufanya sisi tusiwe na uwezo wa kupaingia
mahali patakatifu pa mbinguni ili wakati huu tuweze kupaingia.
“Kwa
hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu
Kwa damu ya Yesu, Kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa Kwa ajili yetu
kupitia kwenye lile pazia, yaani, MWILI Wake”. Waebrania 10:19-20
Njia mpya ya kupaingia Patakatifu
pa Patakatifu tumekwishwa kufunguliwa wakati huu inayopita katika pazia yaani MWILI
wake. Mwili wake ndiyo njia ya kupaingia mahali patakatifu. Elewa vizuri hapa,
hatutumii damu ya Yesu kama njia ya kupaingia Patakatifu pa Patakatifu bali
tunatumia mwili wake kama njia, lakini damu ya Yesu inatupa ujasiri wa kupita
kwenye hiyo njia na kupaingia Patakatifu pa Patakatifu. Ndiyo maana pazia la
hekalu halikupasuka wakati damu yake inatoka bali wakati mwili wake unatolewa
sadaka msalabani – roho yake ilipoachana na mwili wake. Kifo chake ndicho
kilichoifisha dhambi na sisi tukapata nafasi ya kupaingia patakatifu pa
patakatifu.
“Kwa
maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu,
ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa
aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu.” Waebrania 9:24
Yesu alipaingia Patakatifu pa
Patakatifu penyewe pa mbinguni ili aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. Naye
alipaingia kama mtangulizi wetu, mahali hapo ndipo tunapotakiwa kuwa wakati wa
maombi. “Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia (yaani mwili wake) ya
kumkaribia Baba katika Roho mmoja” (Efeso 2:18). Kumkaribia mahali alipo ili
tuonekane mbele zake, kwa maana katika Kristo sisi tuliokuwa mbali hapo kwanza
tumekuwa karibu kwa damu ya Yesu (Efeso 2:13).
KUOMBA KATIKA ROHO
Mungu hatamani wakati unaomba
uombee ukiwa mbali bali anataka ukiwa karibu yaani uonekane mbele zake kazi.
Kwa kuwa Mungu ni Roho basi tunaweza kuonekana mbele zake kwa roho zetu katika
maombi. Wakati wa kuomba sio miili yetu inayohudhuria mbele za BWANA bali roho
zetu. Na ili maombi yawe na matokeo mazuri basi ni muhimu kuomba katika roho.
Nina mkumbuka mama mmoja ambaye alikuwa hana mtoto mda mrefu, ambapo naamini
alikuwa akimwomba Mungu kwa sababu alikwa na kawaida ya kwenda nyumbani mwa BWANA
mara kwa mara. Lakini siku moja alipoenda nyumbani mwa BWANA kama ilivyo
desturi kitu kipya kikatokea alipoona abadilishe namna ya kuomba mpaka kuhani
akafikiri amelewa;- “Basi Hana alikuwa akinena MOYONI mwake, midomo yake tu
ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe, kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa
amelewa……..Hana akajibu….nimeimimina roho yangu mbele za BWANA” 1 Samweli
1:13-15
Hana midomo yake haikutoa sauti
lakini moyo wake ulikuwa unapaza sauti mbele za Mungu, Moyo wake ulikuwa mbele
za Mungu ukiomba, akiwa ameumimina moyo wake. Hana aliyafanya mambo mawili;
kuomba kwa roho na kuomba kwa moyo wake wote. Kuomba kwa moyo wote ndiyo maana
ya kuumimina moyo kwa Mungu. Hii ndiyo inayoonesha kwamba unachokiomba
unakihitaji kwa moyo wako wote. Sio nusu unahitaji nusu hauhitaji.
Tunatakiwa kuelewa kwamba
kinachoingia katika madhababu ya mbinguni, sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu
sio mwili bali roho. Roho zetu ndizo zinatakiwa zionekane mbele za Mungu
zikiomba. Ndio maana hapo juu nilikuwa najaribu kukuonesha wapi tunasimama
wakati wa kuomba (where we stand in prayers) mbele za Mungu. Kwa hiyo kila
unapotaka kuomba, hakikisha kwamba unaonekana mbele za Mungu kwa roho yako
katika Patakatifu pa Patakatifu.
Kuomba kwa roho haimaanishi ni
kunena kwa lugha tu, unaweza usinene kwa lugha na roho yako ikawa inaomba.
Kinachotakiwa unachokiomba kiwe kinatokea rohoni mwako.
“Bali
wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango
wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini
atakujazi” Mathayo 6:6
Zaburi
ya 91:1 inapotuambia “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika
uvuli wake Mwenyezi” tunapata kujua kwamba mahali pa
“siri” ni mahali pa makao ya Mungu au uweponi mwake. Mtu anapoambia “...Usalipo
mbele za Baba yako aliye siri...” ni wazi kwamba yeye mwenyewe anahitajika
mahali hapo pa “siri” ili aweze kuomba mbele za Baba. Kwa sababu huwezi kuwa mbele
za mtu na usiwepo mahali alipo. Hapo mahali pa “siri”, roho tu ndiyo inaweza
kuhudhuria na sio mwili. Kwa hiyo anaposema “ingia katika chumba chako cha
ndani” anamaanisha kuwa katika roho yako na kusahau kwa mda habari ya mambo ya
mwili. Kuachana na fikra, mawazo, na chochote kinachoweza kukuzuia kuwa mbele
za Mungu kuomba. Hiki ndiyo alichokuwa anakifanya Hana alipokuwa akiomba. La
muhimu ni kuhakikisha kwamba unakuwa na mazingira mazuri ya kuomba.
KUNENA
KWA LUGHA
Ingawa
hata usiopo omba kwa kunena kwa Lugha, lakini ni muhimu sana mtu kwa mtu kuomba
kwa kuneno kwa Lugha. Najua wako wengine ambao hawaamini katika kunena kwa
lugha lakini nachojuaribu kuelezea hapo ni kile neno la Mungu linatufundisha.
Kuna
mambo kadhaa nataka uone:-
Mtu
anaponena kwa lugha, roho yake huomba kwa Roho mtakatifu, ikiwa na maana yale
maneno anayojaliwa mtu kutamka, ni kwa roho yake yanatamkwa. Kwa hiyo mtu
anakuwa na uhusika wa moja kwa moja.
“Maana nikiomba kwa lugha, roho
yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda”
1 Wakorintho 14:14
Akili
inakuwa haielewi kile ambacho roho inaomba lakini roho yenyewe inaelewa na
Mungu pia anaelewa. Kumbuka kwamba yale maneno yanayotamkwa yanakuwa na msukumo
wa Roho mtakatifu. Kunena kwa lugha ni njia moja wapo ya kufunga milango
uingiapo sehemu ya ndani. Mambo yote yanayokuwa yanaendelea akili zako zinakua
hazielewi hii inaifanya kutuliza akili zako.
Kwa
kunena kwa Lugha, unapata nafasi ya kuyaombea mambo ya siri yaliyofichika.
“Maana yeye anenaye Kwa lugha,
hasemi Na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo
ya siri katika roho yake” 1 Wakorintho 14:2
Kuna
wakati ambao, akili zako haielewi wala kujua baadhi ya mambo lakini roho yako
inayajua na kuyaelewa. Unaweza tu kuomba kwa lugha ya kibinadamu pale tu akili
ya mtu inapoweza kulielewa jambo. Kwenye
mstari huu tunaona kwamba yeye ananaye kwa lugha hasemi na watu bali anasema
moja kwa moja na Mungu kwa roho yake. Pia tunaona kwamba ananena mambo ya siri
ikiwa na maana ya mambo yaliyofichika katika akili za kibinadamu. Kuna mambo
ambayo roho yako inakuwa imeyaona lakini akili yako bado haijayaelewa. Kwa kunena
kwa lugha, unaweza kuyaombea hayo mambo hata pale ambapo akili yako inakuwa
bado haijayaelewa na Mungu akashughurikia.
Kwa
kunena kwa lugha, unaweza kupata ufahamu juu ya mambo ya sirini usiyoyajua
bado. Mtu anaponena kwa lugha, roho yake huomba katika Roho mtakatifu, yaani
Roho mtakatifu hushiriki pamoja na roho yake kuombea hayo mambo ya siri, huku
akili zikiwa hazina matunda. Lakini kwa kadiri anapoendelea kuomba, Roho
mtakatifu anayafunua hayo mambo ya siri ili aweze kupata ufahamu juu ya mambo
hayo. Ukisoma mithali 20:27 inasema “Pumzi (roho) ya mwanadamu ni taa ya Bwana;
Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake”. Utagundua kwamba Mungu huitumia roho ya
mwanadamu kama taa kuyamulika yote yaliyofichika ndani yake. Roho itapeleleza
yote ambayo hayajajulikana bado ili kuyafunua yaje nuruni yajulikane. Kwa njia
hii inaweza kuyajua hata na mafumbo ya Mungu.
Kunena kwa Lugha
kunaijenga nafsi na kuiimarisha
“Yeye anenaye kwa
lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa”. 1 Wakorintho 14:4
Biblia iko wazi kwamba yeye
anenaye kwa lugha anafanya kazi ya kujijenga na kujiimarisha mwenyewe lakini
yeye anayehutubu analijenga kanisa, kwa hiyo unapotaka kujijenga roho yako,
jizoeshe kunena kwa lugha mara kwa mara, kwa sababu hii pia inasaidia kukupa
uwezo na nguvu za kuomba kwa muda mrefu, na unapotaka kulijenga kanisa, ni
muhimu ujizoeshe kuhubiri na kufundisha neno la Mungu mara kwa mara ili liweze
kufaidi katika maneno utakayoyasema. Omba mara kwa mara kwa kunena kwa lugha,
ili uweze kupata faida hizi na kuimarisha roho yako.
Kukua na kuimarika rohoni
inauhusiana mkubwa na kumjua Mungu au kuwa na ufahamu na maarifa juu ya elimu
ya utukufu wa Mungu. Hata hivyo kuwa na ufahamu na maarifa katika Mungu ni
kigezo kimoja wapo kujua kwamba umekua na kuimarika. Biblia inasema “Lakini,
kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu
una yeye sasa na hata milele.” (2 Petro 3:18). Tunatakiwa
kukua na katika kujua Bwana yaani kupata maarifa na ufahamu juu ya elimu ya
Mungu ambavyo tunafahamu kama ufunuo (revelation) kutoka kwa Mungu. Hii hazina
inajazwa ndani yetu kwa njia ya roho ya ufunuo. Kwa maombi ya mara kwa mara
yanatuweka mahala pazuri kwa roho zetu kupata ufunuo.
Paulo alitamani watu wa Efeso
waweze kukua na kuimarika katika kumjua Mungu, akawaombea roho ya ufunuo na
roho ya hekima. Hekima ni muhimu ili waweze kutumia ipasavyo ufunuo wanaoupata.
Hakuna namna utaweza kupata ufunuo wa kumjua Mungu katika neno lake bila maombi
ya mara kwa mara. Unapoendelea kuomba mara kwa mara tena kwa bidii, ndipo
utaanza kuona unaanza kulielewa neno la Mungu na kupata ufunuo ndani yake. Naamini
siri hii ya maombi ndiyo iliyomsaidia Paulo kuelewa maandiko ya agano la kale kwa
picha ya agano jipya.
Jiombee na wewe mara kwa mara sara hii ambayo Paulo aliwaombea Waefeso
baada ya muda utashangaa uelewa na ufahamu wako wa mambo ya rohoni unaongezeka
na kuwa mkubwa. Maombi ya namna hii ndiyo yaliyomsaidia Daudi kupata ufahamu
juu ya mambo yaliyokuwa yanamchanganya kwa sababu aliyokua hayajui na yaliyokuwa
hayana majibu kwa jinsi ya kibinadamu. Mfano, juu ya ukame ulioikumba nchi yake
(2 Samweli 21:1), pia kuhusu kufanikiwa kwa waovu (Zaburi 73:16-18). Mambo haya
yalimsumbua sana Daudi, lakini ufumbuzi aliupatia kwenye maombi. Yafanye maombi
kama sehemu yako, penda kuomba.
Endelea kufatilia mundelezo wa
somo hili, Mungu akubariki
NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO- 6
Reviewed by Unknown
on
3:58:00 PM
Rating:
No comments: