BREAKING NEWS

[5]

NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -4





NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -4

Karibu tuendelee na mwendelezo wa somo letu la namna ya kukuza na kuimarisha roho yako, na kwa sasa tunaendelea na jambo la pili kuhusiana na kuabudu.



2.    Aabuduye anatakiwa kuwa katika ngazi ya mwana, na Mungu kama baba
Hili ni jambo la muhimu kulielewa, kwa sababu linaenda kwenye kiini cha shughuri yenye ya kuabudu. Yesu anamwambia yule mama msamalia kwamba “…. Waabuduo halisi watamwabudu BABA katika roho na kweli….” Kila mara Yesu anapomtaja Mungu kama baba yake anatamani na sisi tumwone hivyo wakati huo, ona mstari wa Yohana 20:17 Yesu alipokuwa anazungumza na Mariamu;

Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba, Lakini enenda kwa ndugu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, Kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu”  Yohana 20:17

Anamwambia Mariamu kwamba asimguse kwa sababu bado hajaenda kwa Baba yake ambaye pia ni baba yao, kwa kusema vile Yesu alitaka Mariamu atambue kwamba alikuwa anakwenda kwa Baba yao wote ili hata wakati mwingine akisema Baba awe anajua ndani yake kwamba naye ni baba yake.

Kwa hiyo Yesu anaposema waabuduo halisi watamwabudu BABA, alikuwa na maana kwamba hao waabuduo halisi wataenda mbele za Mungu katika uhusiano wa BABA-MWANA wakati wa kuabudu. Hao waabuduo kama watoto na Mungu kama Baba. Hili ni jambo muhimu kulielewa kwa kila anayetamani kumwabudu Mungu.

Hii ni kwa sababu kadhaa, ya kwanza ni kwamba hatumwabudu Mungu tukiwa mbali, bali karibu. Imeandikwa kwamba watamwabudi katika roho, ikiwa na maana roho zetu ndizo zitakazoonekana mbele za Mungu kuabudu. Mahali alipo tuwepo hapo kuabudu. Tunaweza kupata nafasi ya kumkaribia Mungu kwa roho, kwa hiyo roho zetu zinatakiwa ziwe na upenyo (acces) wa kumfikia Baba. Jambo la pili, Baba maana yake chanzo, mwenye kuuwezesha na kuutunza uzima. Pale tu mtu anapokuwa ameungwa na chanzo chake yaani Mungu ndipo anapoweza kuachilia ibado iliyosahihi inayokubalika.

Yahana anatusaidia namna ambavyo tunaweza kupata upenyo wa kumfika Baba na kufanyika watoto wa Mungu;

Bali wote waliompokea aliwapo uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12)

Wale wote wanampokea (kuzaliwa mara ya pili) hao wanapewa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, Mungu anakuwa ni Baba yako na Roho mtakatifu huja kushuhudia pamoja na roho zetu kwamba tu watoto wa Mungu na kulia Aba yaani Baba. Sasa kutokea kwenye nafasi hiyo ndipo tunapoweza kumwabudu Mungu ipasavyo. Hii ni kwa sababu kwa kufanyika mtoto, roho ya mtu inaungwa na na kuwa karibu na Roho ya Mungu. Huwezi kuabudu kitu usichoungwa nacho roho na tunaungwa roho zetu na Mungu kwa kuzaliwa mara ya pili. Kwa hiyo kama hujazaliwa mara ya pili, huna muunganiko naye wala huwezi kuwa karibu naye. Kama unatamani kuwabudu Mungu ipasavyo, basi fanya bidii ukazaliwe mara ya pili ili upate hiyo nafasi. Mungu hatamani tumwabudu mioyo yetu ikiwa mbali naye wala tumwabudu tokea mbali.

Bwana anasema: “ kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami. Huniabudu bure, mafundisho yao ni sheria tu walizofundishwa na wanadamu. (Isaya 29:13)

Ona hapa, Mungu anasema watu hawa huniabudu bure (bila faida/matunda) kwa sababu mioyo yao iko mbali naye ingawa wanasema kwa vinywa vyao. Mungu hujali sana moyo kuliko uyasemayo, na anataka moyo wako ndiyo useme mbele zake wala sio mdomo tu. Kwa kuzaliwa mara ya pili tunapata nafasi ya kumkaribia na kuungwa na Mungu.

3.      Muda wa kuabudu ni sasa
Hili ni jambo la tatu la muhimu tunaloliona kwenye mstari wa Yohana 4:23. Tokea hapo tunaona kwamba muda wa kuabudu ni sasa. Ili kuelewa vizuri jambo hili naomba tuusome tena.

Lakini saa inakuja, tena sasa ipo, ambayo waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu (Yoh 4:23)

Yesu alikuwa akiongea na mama msamalia kwamba, saa inakuja ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Na Mungu anawatafuta watu kama hao. Naomba nisome kwa staili nyingine lakini bila kuharibu maana ya mstari huu wa Yohana kwa kuanzia chini alafu nitaacha neno moja ambalo nitalirudishia tena ili kuelewa vizur. Inaweza kuandikwa kwamba “Kwa kuwa Baba anawatafuta waabuduo halisi, basi saa inakuja ambayo hao waabuduo, watamwabudu Baba katika roho na kweli” Yesu alikuwa anamwambia, hey mama, Mungu yuko anatafuta watu watakaoweza kumwabudu katika roho na kweli, kwa hiyo ni hakika kwamba sasa inakuja ambayo kuanzia hapo itaanza kutumiwa nao waabudu halisi watakaopatikana na Mungu. Yesu alikuwa akisema akiisha kuwapata, wataanza kumwabudu Baba. 

Hii inatupa uhakika kwamba hiyo saa ni hakika kwa sababu Mungu hatakosa kujitwalia watu wa namna hiyo. Yesu alikuwa akimtaadharisha yule mama kwamba, jiandae na wewe ukitaka ili itakapofika hiyo saa nawe uwemo katika ya wale watako mwabudu Mungu katika roho na kweli. Kwa kusema vile alikuwa anaamsha roho ya yule mama akaye mkao wa kusubiri hiyo saa kiasi ambacho kinaweka uhitaji wa kitu ndani yake. Maana ukitazama jambo lenyewe lilivyozuri na kwamba Mungu yuke busy kutafuta, inakupa kiu kwamba nami niwemo na saa hiyo ifike. Na kama Mungu anatafuta watu, basi ujue anavigezo vyake anavyoviangalia ili uweze kuwa mmoja wao. Kwa hiyo inatakiwa kujiandaa kiasi ambacho wakati huo ufikapo haupitwi na Mungu wala haukosi kuabudu. Maana kukutana na Mungu inahitaji maandalizi. Lakini ona Yesu anachokisema “….., tena sasa ipo,…” kwa hiyo anaivuta saa itakayokuja na kuileta sasa. Saa hiyo ambayo anasema inakuja, imekwisha kutimia sasa. Wale waabuduo halisi wanaabudu sasa kwa sababu saa yao imeshatimia tayari. Inawapasa na wanaabudu sasa. Kila wakati unaoitwa sasa, ni wakati wa kuabudu. Hii inamaanisha kwamba kila kipande cha muda unachobaatika kukiishi ni wakati wa kuabudu. Maandalizi yote uliyoyafanya yalikuwa ni kwa ajili ya sasa wala sio baadaye wala kesho. Kwa kuwa tunamwabudu Mungu kwa roho zetu basi roho zetu zinatakiwa kuwa tayari na kuunganika na Mungu muda wote ili iweze kuabudu muda wote.

Unaweza ukawa upo kimya kwa jinsi ya nje lakini roho yako inaimba na kumwabudu Mungu. Liakiwalo kujua ni kwamba huu (sasa) ndio wakati wa kuabudu, hatumuabudu Mungu kwa masaa wala kwa vipi lakini wakati wote mioyo yetu iwe mbele zake ikitoa ibada. Mungu haitaji ibada yako leo alafu kesho upumzike, sasa hivi alafu baadaye upumzike. Ibada ni zaidi ya kukusanyika kwenye nyumba za ibada kuabudu, Ibada inahusu moyo wako na huo anauhitaji mbele zake wakati wote utoe ibada.

Kwa namna hii inatufanya tuonekane mbele za BWANA na kukaa naye wakati wote. Kwa kadiri unavyoendelea kuwa mbele zake ndivyo unavyoendeleakuwa kupokea nguvu na kujenga uhusiano na Mungu zaidi. Unavyoendelea kukaa karibu na Mungu katika ibada, inatengeneza nafasi ya Mungu kuachilia tabia zake ndani yako na baada ya mda utajikuta tabia za kiuungu zinaumbika ndani yako.

Ili kufanikiwa kwenye eneo la kusifu na kuabudu, moyo wa mtu unatakiwa kuwa na kiu na tayari kutekeleza jambo hilo. Mioyo wake uwe karibu na Mungu kuliko hata mwili na mdomo wake. Maana moyo wake ukiwa mbali, kuabudu kwake hakuna faida.

Bwana anasema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao na kuniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Huniabudu bure, mafundisho yao ni sheria tu walizofundishwa na wanadamu” Isaya 29:13   

Mungu anasema watu hawa wananiabudu bure, maana yake wanaabudu bila faida. Lakini inatakiwa kuabudu kwa faida na faida moja wapo ni kuimarishwa kwa roho zetu. Mungu anatamani moyo wa mtu ujae ibada na kumheshimu Mungu ndani yao. Tuone mstari wa zabur jinsi unavyoweza kutusaidia.

Heri ni wale ambao nguvu zao ziko kwako, na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao. Wanapopita katika Bonde la Bakaa, hulifanya mahali pa chemchemi, pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi. Huendelea toka nguvu hadi nguvu, hadi kila mmoja afikapo mbele za Mungu huko Sayuni” Zaburi 84:5-7  

Daudi anasema wanaheri wale ambao nguvu zao zatoka kwa Mungu, ambao njia ziendazo sayuni ziko moyo mwao. Sayuni unajulika kama mlima wa BWANA, mahali pake pa kustarehe na watu walikuwa wanamwendea hapo. Lakini ona kitu anachokisema Daudi, njia za kuendea hapo (Sayuni) ziko moyoni mwao. Hizo njia sio tu kwamba huwa wanazipita kumwendea Mungu huko bali ziko mioyoni mwao. Wanazipita njia ambazo ziko mioyoni mwao tayari. Wanapokuwa wanazipita kwa jinsi ya mwili wanakuwa washazipita mioyoni mwao tayari. Mungu huwaanataka unalolikusuduia Moyoni ndilo ulitekeleze, hilo ndilo lenye faida/ matunda.  Tafsiri ya kiingereza ya AMPLIFIED BIBLE inasema “...in whose heart are the highways to Zion..” Mungu anahitaji watu ambao wataweka njia kuu mioyoni mwao na watakuwa na kiu na tayari kuiendea njia hiyo. Njia ziendazo sayuni zinatakiwa ziwemo moyoni ili kuweza kuiendea hiyo njia na kufika Sayuni. Kabla ya kufanya ibada mioyo yetu inatakiwa iwe tayari imejaa ibada. Kuwa na kiu na utayari wa kumwabudu Mungu, kunamfanya Mungu akupe nguvu, na kukupitisha sehemu ya chemichemi, na kuongezeka nguvu hata nguvu. Kwa kufanya hivyo Roho zetu huimarika zaidi.
  
Endelea kufatilia mundelezo wa somo hili, Mungu akubariki
NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -4 NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -4 Reviewed by Unknown on 5:54:00 PM Rating: 5

No comments:

Sora Templates