BREAKING NEWS

[5]

NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO- 5



MAOMBI
Baada ya kuangalia kwa undani kuhusu neno la Mungu, kusifu na kuabudu na jinsi kunavyoweza kuimarisha roho yako, ni wakati mzuri sasa kujifunza namna maombi yanavyoweza kuikuza na kuimarisha roho yako. Kama nilivyotangulia kusema, namna hizi zote zinalenga katika kumkaribia Mungu (kuwa karibu na Mungu). Kwa hiyo njia hizi ukizitumia ipasavyo zitakufanya umkaribia Mungu zaidi hatua kwa hatua. Ukaribu huu ndio unaofanya mahusiano kati ya Mungu na mtu kuimarika. Ili kuelewe jambo la maombi namna linavyoweza kuimarisha na kukuza roho yako, ni vizuri kukueleza kidogo maana ya maombi.

Maana ya maombi
Maombi yanatazamwa kwa mtazamo tofauti kwenye biblia. Maombi kwa jinsi ya mwili yanajulikana kama kuhitaji msaada juu ya mahitaji ambayo mtu anayo. Kitu ambacho ni sawa lakini tuangalie biblia inasemaje. Kibiblia maombi yana mitazamo tofauti lakini yote ikimlenga Mungu:-
        a.       Maombi ni mawasiliano baina ya Mungu na mwanadamu
        b.      Maombi ni ushirika (fellowship) kati ya mtu na Mungu
        c.       Maombi ni njia ya kuwasilisha na kupokea mahitaji yetu kwa Mungu

Kwa somo hili tutachukua tafsiri ya kwamba maombi kama ushirika kati ya mtu na Mungu kwa sababu tukienda kwa picha hii na pia tukifanya hivi (fellowship na Mungu) ndipo tunaweza kujenga roho zetu na kuziimarisha.

Inapofika wakati kujenga na kuimarisha roho yako, inapaswa kutanua fikra kuona maombi zaidi ya kuona ni njia ya kupeleka mahitaji yetu kwa Mungu, bali kuona ni sehemu ya ushirika na Mungu. Na Mungu anataka tuone ni sehemu ya ushirika kati yetu na yeye kuliko kama njia tu ya kupeleka mahitaji ingawa mahitaji yetu tunaweza kuyapokea tu kwa maombi pekee.

Namna ya kupokea mahitaji
Biblia iko wazi kwamba kwa maombi pekee tunaweza kupokea mahitaji yetu kutoka kwa Mungu hii ni kutokana na jinsi Mungu alivyotengeneza mfumo wake wa namna ya kumsaidia mwanadamu. Kwa hiyo mtu asipoomba asitegemee kitu toka kwa Mungu. Yakobo 4:2 anatuambia:- “…..wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi”. Ni muhimu sana kujua kwamba vitu kutoka kwa Mungu tunaweza kuvipata kwa njia ya maombi. Kwa hiyo tunaweza kuongeza vitu kutoka kwa Mungu maisha mwetu kwa njia ya maombi. Yeye aliye mvivu kuomba, ndivyo na vitu vya Mungu vitakuwa adimu maishani mwake.

Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa Math 7:7-8

Biblia inatuhakikishia kwamba ombeni nanyi mtapewa, na kila aombaye hupokea. Ona hapa, Mungu anatoa wito wa kuomba juu ya mahitaji yetu, na sentensi hii inatuonesha kwamba tunachokiitaji kipo stoo, ukiomba unapewa. Mungu anamwambia kila mmoja kuwa ukiomba utapewa unachokiomba. Lakini yeye achukuaye hatua ya kuomba, sio kwamba atapewa yeye hupokea. Wakati anaomba ulikuwa sio wakati wa kusema atapewa lakini ni wakati wa kupokea. Kwa hiyo maombi ni njia ya kupokea mahitaji yetu kwa Mungu. Maombi sio tu kwamba tunapeleka mahitaji bali tunapokea mahitaji yetu kutoka mwa Mungu. Kwa sababu kila aombaye hupokea. Hii ni kutokana kwamba tunatakiwa kuomba kwa imani.

Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu Marko 11:24

Omeona hapo? Tunayapokea tunayoyaomba wakati wa kuomba. Hili ni jambo la muhimu kulifahamu. Wengi baada ya kuomba ndiyo wanajiandaa kupokea, biblia haisemi hivyo, inasema “maana kila aombaye, hupokea…” kupokea ni kwa kila anayeomba kama akiomba sawa sana na mapenzi ya Mungu. Kwa njia ya maombi tunapokea tunayoyahitaji, kwa hiyo hakuna maombi hakuna mahitaji. Huo ndio mpango wa Mungu.

Katika kujenga mausianao yetu na Mungu ni vizuri kuona maombi kwa sura nyingine kabisa. Sio tu kwamba maombi ni njia ya kupokea mahitaji yetu bali pia ni sehemu ya ushirika na Mungu. Maombi yanapokuwa kama ushirika kati ya Mungu na mwanadamu, mambo mawili hutokea kwa haraka; moja, mtu ataenda kwenye maombi sio kwa sababu ana mahitaji tu na pili, huyo mtu haitamsumbua hata asipopata analichokuwa anakiomba kwa sababu gafla uhusiano wake na Mungu unakuwa haujengwi katika mahitaji anayoyaomba bali katika upendo na ushirika dhabiti. Kuona maombi kama njia ya kujenga na kuimarisha ushirika na Mungu ni bora zaidi kuliko kuona maombi kama njia ya kupokea mahitaji yetu kwa sababu, kigezo kimojawapo kinachomfanya Mungu kukupa unachokiomba ni mahusiano (ushirika) mazuri kati yako na yeye. Kwa kadiri unapoendelea kujenga ushirika naye ndivyo na hofu (kumcha) yake inavyozidi kujengeka ndani yako.

“Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti,maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, na akasikilizwa kwa ALIVYOKUWA MCHA MUNGU” Waebrania 5:7

Mstari huu unazungumza kwa habari ya Yesu Kristo alipokuwa katika mwili. Alimtolea Mungu maombi na dua pamoja na kulia na machozi, lakini alisikilizwa na kujibiwa sio kwa sababu tu aliomba na kulia na machozi bali kwa sababu alikuwa mcha (hofu ya) Mungu. Maombi, dua na machozi yana nafasi yake, lakini wakati mwingine kama uhusiano wako na Mungu sio mzuri kuna mambo huwezi kupata. Mungu anaweza kusikia maombi yako na kuyaona machozi yako na kukujibu kama mfalme Hezekia (2 Wafalme 20:5).
Ni vizuri mtu akalenga katika kuimarisha mahusiano yake na Mungu katika maombi ili kuhakikisha kwamba kila analoliomba analipokea. Ili kufanikisha kujenga mahusiano na Mungu ni vizuri kukumbuka mambo kadhaa, la kwanza, Mungu ni Roho kwa hiyo unaweza kuwasiliana naye kwa roho yako, la pili, maombi hufanyika rohoni (moyoni) yaani mtu anapaswa kuomba kwa moyo wake wote iwe akili zake zina matunda ama hazina matunda.

Kutengwa na uso wa Mungu
Wakati wa maombi ni wakati wa kuonekana mbele za Mungu kabisa na kuzungumza naye, yaani roho yako inakutana na Roho ya Mungu katika maombi. Niweke wazi kwamba mara baada ya Adamu kufanya dhambi ilitutenga na uso wa Mungu.

Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:17

Mungu alimtahadharisha Adamu kwamba usile hayo matunda na siku utakapokula hakika utakufa, neno “utakufa” lilikuwa halimaanishi kufa kwa jinsi ya mwili bali kwa jinsi ya rohoni yaani kutengwa na uso wa Mungu.gafla macho ya Adamu ya rohoni yakafungwa yasiweze kuona mambo ya Mungu na macho ya mwilini kufunguka. Akawa mbali na Mungu kwa sababu ya dhambi, makosa na uovu juu ya Mungu. Ushirika na ukaribu wa Mungu kwa Adamu ukawa hakuna tena, Adamu alikuwa hawezi kuzungumza na Mungu kama mwanzo ilivyokuwa.

Lakini maovu yenu yemewafarakanisha ninyi Na Mungu wenu, dhambi zenu zimeuficha USO wake msiuone, hata hataki kusikia” Isaya 59:2

Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na mikutano ya ibada, siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu. Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi na sikukuu zenu zilizoamriwa moyo wangu unazichukia. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia. Mnaponyosha mikono yenu katika kuomba, nitaficha macho yangu nisiwaone, hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. Mikono yenu imejaa damu” Isaya 1:13-15

Madhara ya makubwa ya dhambi ni kututenga na Mungu, hata tusiweze kuuona uso wake. Maana dhambi zinatuficha mbali na uso wa Mungu. Adamu kukimbilia sehemu ya kujifisha ilikuwa ndicho kilichotokea na alichokuwa anajisikia rohoni kwa wakati ule. Ile kukimbia ilikuwa ni ishara ya kitu kilichotoa rohoni mwake. Ndio maana hata sasa ukifanya dhambi hasikii ndani yako kukaa karibu na Mungu na unajisikia kukaa mbali. Kwa sababu mtu hujisikia kuhukumiwa kila wakati. Hata kama alikuwa anafanya kwa siri, gafla utakuta haunekani alipokuwa anapatikana siku zote, mahali pa maombi, kusifu na kuabudi, kusoma neno n.k. Hii ni kwa sababu kila akiomba, haoni akijibiwa, akiinua mikono yake, Mungu anauficha uso wake.

Lakini Mungu alichokikusudia tangu mwanzo tunakiona pia katika Zekaria 3:7 anapotuambia;

BWANA wamajeshi asema hivi, kama ukienda katika njia zangu na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya KUNIKARIBIA kati yao wasimamao karibu
 
Nijaribu mfano huu, kuna wakati wanandoa wanaweza wakawa hawaishi nyumba moja kutokana na majukumu ambayo kila moja anakuwa nayo (safari za kikazi, au kuhama kikazi) ingawa ni hakika wanatakiwa kukaa nyumba moja tena chumba kimoja zaidi sana kitanda kimoja. Katika hali hizi zote mbili, wanatakiwa kuwa karibu sana kimahusiano kwa sababu wameshakuwa mwili mmoja. Ingawa Mungu anahitaji mahusiano ya karibu sana na wanadamu lakini pia anakuhitaji mahali alipo karibu sana naye, madhabahuni, mbele ya kiti cha enzi mbinguni. Kusudia la Mungu ni kwamba mwanadamu awe anakaribia mbele za kiti chake cha enzi wakati wote, ndiyo maana hapo anamwambia Yoshua kuhani kwamba kama ukifuata maagizo na njia zangu (akiachana na dhambi na uovu), nitakupa nafasi ya kukaribia mbele zake. Anaposema “nitakupa nafasi” inatuonyesha wazi kwamba kuna “nafasi” ya wanadamu mbele za kiti cha enzi iliyowekwa na Mungu ambayo dhambi imeifanya hiyo nafasi kuwa wazi kwa sababu wanadamu wakawa hawezi tena kukaribia hapo.

MAHALI PATAKATIFU
Katika harakati za kurudisha kile ambacho Adamu alikipoteza hatimaye na wote waliozaliwa naye kupoteza (nafasi ya kukaribia mbele za Mungu), Mungu anaamua kumwambia Musa kujenga hema sawa sawa na alivyomunesha katika mlima. Hii hema ilikuwa ni picha ya mahali patakatifu pa mbinguni. Akamwambia hivi;-

“Simamisha Hema sawasawa na ramani uliyoonyeshwa kule juu mlimani, Tengeneza pazia la nyuzi za buluu, za zambarau na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, fundi stadi atarizi makerubi kwenye hayo mapazia. Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha. Ning’iniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu. Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya sanduku la Ushuhuda ndani ya Mahali Patakatifu pa Patakatifu” Kutoka 26:30-34

Hema hiyo ilikuwa na sehemu kuu tatu, sehemu ya kusanyiko la Israeli, patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu. Patakatifu pa Patakatifu palikuwa panatengwa na Patakatifu kwa pazia. Hapo palikuwa panahudhuriwa na kuhani mkuu tu. Ilikuwa ndiyo sehemu ya ndani kabisa ya hema, sanduku la ushuhuda (agano), na kiti cha rehemu juu ya hilo sanduku. Na makerubi yaliyokuwa yanafunika kiti cha rehema kwa mbawa zao. Ndipo palipoitwa mahali patakatifu na pa kukutania. Hapo mahali ndipo Mungu alipokuwa amemwambia Musa atakuwa akisema naye.

Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo NITAKUTANA nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu Kutoka 30:36

Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele ya BWANA. Hapo ndipo NITAKAPOKUTANA na ninyi na KUSEMA nanyi, Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu Kutoka 29:42-43

Weka hiyo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya Sanduku la Ushuhuda, mahali ambapo nitakutana nawe Kutoka 30:6

Katika mistari hii yote, ni vyema kuona kwama mahali patakatifu palikuwa na madhabahu, sanduku la ushuhuda na kiti cha rehema kilichowekwa juu ya sanduku la ushuhuda, hapo ndipo Mungu alipokuwa anakutana nao na kusema nao. Kutokea kwenye mistari hii tunaona mambo mawili ya haraka. La kwanza, sio mahali popote pa hema ya kukutania Mungu alikuwa akisema bali kutokea sehemu ya patakatifu pa patakatifu palipokuwa na kiti cha rehema, la pili wale ambao walikuwa hawa nafasi ya kupaingia patakatifu yaani kusanyiko la Israeli walikuwa wanasubiri kuhani aliyekuwa na hiyo nafasi aje awaambiye alichosema Mungu. Kusanyiko lote la Israeli lilikuwa halina nafasi ya kukaribia patakatifu pa patakatifu kwa sababu ya pazia.

Watu wengi pia tunaishi maisha haya kama kusanyiko la Israeli, hawataki kuomba, wanasubiri waombewe na kuletewa majibu na wengine. Na maisha yao yanakuwa tofauti na wale wanaoingia pale patakatifu pa patakatifu. Kila wakati ambao Musa alikuwa anataka kuongea na Mungu alikuwa akienda ndani ya pazia mbele ya kiti cha rehema, na Mungu alikuwa akisema naye kutokea hapa. Musa alijua huo ndio utaratibu ambao Mungu amejiwekea kuwasiliana na mimi baada ya kusimamisha hema ya kukutania. Musa alifanyia maombi yake hapo, kwenye hiyo madhabahu na mbele ya kiti cha rehema baada ya kupita kusanyiko la Israeli na patakatifu. Nilitaka uone mahali ambapo akina Musa walikuwa wanatolea maombi yao na kuzungumza na Mungu. Mungu alitamani kuzungumza nao akiwa karibu.

Barikiwa na endelea kufatilia mwendelezo wa somo hili, karibia tunafika mwisho.
NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO- 5 NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO- 5 Reviewed by Unknown on 10:44:00 AM Rating: 5

1 comment:

Sora Templates