BREAKING NEWS

[5]

NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -1

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli” (Luka 1:80)


Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima na neema ya Mungu ilikuwa juu yake (Luka 2:40)

kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiogoshiwa, ili kwa hayo mpata kuukulia wokovu (1Petro 2:2)
Ukisoma mistari hii na mingine mingi katika biblia unaona wazi kwamba mtu anahitaji kukua rohoni na kuongezeka nguvu kwa sababu anazaliwa akiwa mchanga rohoni (immature). Mistari hii inatuonesha wazi kwamba mtu anatakiwa kukua sio tu mwili bali na roho yake pia, kukua rohoni sio tu kwamba kunaongeza nguvu bali kunaongeza hekima ndani ya mtu na neema juu yake. Mafanikio ya mtu yanategemea sana mafanikio mazuri ya roho yake.
Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama roho yako ifanikiwavyo (3 Yoh 1:2)

Hapo tunaona wazi kwamba Mungu anataka tufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya lakini kwa kadiri ambavyo roho zetu zinafaniwa. Kwa maneno mengine ni kwamba kiwango cha mafanikio ambacho mtu anakifikia ni matokeo ya kiwango cha hali ya kiroho aliyoifikia. Kusudio la Mungu ni tufanikiwe katika maeneo yote ya maisha sio tu machache, sio unafanikiwa maswala ya kiuchumi halafu ndoa inakushinda, au unafanikiwa kielimu halafu sehemu ya kazi unashindwa. Ukweli ni kwamba, roho ya mtu inapofanikiwa katika eneo fulani, matokeo yake yanaonekana kwenye ulimwengu wa mwili kwenye eneo hilo.
Kinachotakiwa ni kwamba mtu awe na ufahamu na nguvu za kutawala mazingira yake. Na kwa sababu ulimwengu wa mwili uliumbwa kutoka ulimwengu wa roho, kutawala mazingira ya ulimwengu wa mwili hainabudi kutawala ulimwengu wa roho kwanza ambao ndio unazaa mambo ya ulimwengu wa mwili. Ulimwengu wa roho maana yake ni eneo ambalo roho pekee ndizo zinazoenenda na kuishi huko. Ingawa roho yako iko ndani ya mwili lakini inaishi ulimwengu wa roho kwa hiyo mtu anaishi katika ulimwengu zote mbili kwa wakati mmoja. Mwili katika ulimwengu wa mwili na roho katika ulimwengu wa roho. Nafsi ndiye kiunganishi na mtafsiri kati ya roho na mwili. Kwa hiyo roho ya mtu inatakiwa iwe na ufahamu na nguvu ya kuutawala ulimwengu wa roho ili aweze kuutawala ulimwengu wa mwili. Kile ambacho unakiitaji (afya, ndoa, uchumi n.k) katika ulimwengu wa mwili inatakiwa roho yako iwe na nguvu ya kukifuata na kukiumba katika ulimwengu wa roho. Hii inakupa sababu ya kufikiri sana habari ya rohoni kuliko ya mwilini kwa sababu ya rohoni ndiyo yanayozaa ya mwilini.

Kwa kuwa ile nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani (Rumi 8:6) 

Kufikiri sana habari na mambo ya mwilini kunamfanya mtu mwili wake kuwa na nguvu na kuyafanya hayo kuliko roho yake, ambao nia yake ni mauti. Lakini nia ya roho ni uzima na amani, kwa hiyo ili uzima na amani vitokee, roho inatakiwa kuwa na nguvu kuliko mwili. Mauti imezwe na uzima. Ili magonjwa yamezwe na uzima, roho ya mtu haina budi kuwa na nguvu na kuwa imara kuliko mwili wake unaoumwa. Kuna mambo ambayo mwanadamu hataweza kuyapata na kuyafurahia hata kama ni yake kwa sababu tu ni mchanga kiroho (Galatia 4:1-2) na hana nguvu rohoni.


Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa, Ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka (Math 11:12)

Maana ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho mtakatifu (Rumi 14:17)
Shetani hata ruhusu kirahisi upate haki, amani na furaha ingawa ni mambo ya ufalme wa Mungu (ufalme wenyewe) ambayo ni stahiki yako, lakini aliye na nguvu huvipata kwa nguvu, asiye na nguvu hawezi kuvipata hivyo. Somo hili linakuja kwako upate kiu ya kuongeza msuli katika roho ili uweze kuvipata vile ulivyokuwa unavikosa.
Kuna mambo manne ya msingi ambayo kila mtu atakaye kukua, kuimarika na kuongezeka nguvu kiroho hana budi kuwa nayo na kuyafanya kwa sababu hayo ndiyo chanzo na msingi wa kuimarika kiroho. Mambo hayo ni neno la Mungu, maombi, kusifu na kuabudu, ushirika na watakatifu. Mambo haya yote yanalenga kufikia jambo moja tu muhimu, kumkaribia Mungu zaidi. Mungu kuongezeka Ukuu moyoni.
Wakati fulani Yohana mbatizaji aliposikia habari za Yesu alisema maneno haya “Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi KUZIDI, bali mimi kupungua” (Yoh 3:30). Hii inampasa kila mtu anayezaliwa mara ya pili kuona kwamba Mungu anatakiwa azidi moyoni. Ukiwa safarini kwa gari, kwa mbali mlima unaonekana ni mdogo lakini kadri unavyoukaribia ndivyo na ukubwa wake unaongezeka kwenye upeo wa macho. Kiuhalisia sio kwamba ule mlima unaongezeka ukubwa bali kwa sababu ya upeo wa macho ya mtu. Ndivyo ilivyo tunapofanya bidii kumkaribia Mungu. Ingawa Yeye ni Yeye Yule habadiliki, lakini Ukuu wake huongezeka ndani yetu kwa kadiri tunavyozidi kuwa karibu naye.
Hapa nitakuwa nachambua jambo moja baada ya jingene kwa undani ili kuona ni namna gani kila moja linasaidia kukuza na kuimarisha roho yako.


NENO LA MUNGU

Ili kuelewa neno la Mungu vizuri na jinsi linavyofanya kazi katika kukuza na kuimarisha roho ya mtu, kuna mambo kadha wa kadha ambayo ni ya muhimu na msingi kuyafahamu na kuyafunga katika nia za viuno vyetu. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:-


Jambo la kwanza

Neno ni Mungu mwenyewe. Hili ni jambo la msingi kulifahamu na kulishika kwa kila mtu anayetaka kufanikiwa kiroho kwa sababu linajenga picha halisi ya neno la Mungu.

Hapo mwanzo, alikuwako Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1)

Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye Yeye aliyempanda huyo farasi aliitwa Mwaminifu na wa Kweli. Yeye ahukumu kwa haki na kupigana vita. Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa Chake kuna taji nyingi. Alikuwa na jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu ye yote anayelijua isipokuwa Yeye mwenyewe. Alikuwa amevaa vazi lililochovywa kwenye damu na Jina lake ni ‘‘Neno la Mungu.’’  (Ufunuo 19:11-13)

Mistari hii miwili inamuelezea Mungu kama neno kwa wazi zaidi. Yoh 1:1 inaeleza kwamba NENO ndilo lililokuwapo tangu mwanzo na yeye NENO ndiye Mungu. Na Ufunuo 19:11-13 inaeleza kwamba kuna jina limeandikwa. Mistari hii yote miwili inaweka wazi kwamba YESU ndiye NENO na ndiye Mungu. Hii inasadia kujenga imani na msimamo ndani ya moyo wa mtu kwamba, kila unaposoma neno na kulitafakari, unasoma na kumtafakari Mungu mwenyewe. Pale mwanzo nilisema njia zote tano za kukuza na kuimarisha roho yako zinalenga katika kumkaribia Mungu na kuongezeka ndani, kwa hiyo yeye huongezeka kwa kadiri unapomsoma na kumtafakari katika neno ambalo ndiyo yeye Mwenye.


Jambo la Pili

Neno ni Roho

Ieleweke wazi kwamba neno ni Roho ikiwa na maana ya Roho mtakatifu lakini pia ikiwa na maana ya kwamba linamakao katika ulimwengu wa roho. Kuna wakati fulani Yesu alipokuwa akiongea na mafarisayo na masadukayo, walishindwa kumwelewa akiwa anajizungumzia yeye kama mkate wa uzima na wanafunzi wake pia hawakumwelewa ikabidi wamuulize, Yesu akajibu kwamba Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima (Yoh 6:63). Paulo pia aliandika kwambaYeye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya, si wa andiko bali wa roho, kwa maana andiko huua bali Roho huhuisha (hutia uzima)” (2Kor 3:6) 
Kuelewa kwamba neno ni roho ni Muhimu sana. Inakupa kuelewa kwamba unapolipokea neno hulipokei na kuliweka mwilini bali rohoni ili kuleta matokea katika mwili. Ukweli ni kwamba hakuna kitu chochote kinachoweza kufanyika mwili isipokuwa roho. Biblia inaposema kwamba “Naye Neno alifanyika mwili.” (Yoh 1:14) ina maana kwamba Neno ambaye ndiye Mungu ambaye ndiye Roho ndiye ambaye alifanyika mwili. Kwa sababu “…..Bwana' ndiye Roho”(2 kor 3:17).

Uzima uko ndani ya roho. Uzima wa kitu chochote uko ndani ya roho yake hiyo kitu. Ili hicho kitu kiihuike kinahitaji uzima ndani ya roho yake. Na roho iliyo na uzima imefichwa ndani ya neno. Na neno linapotamkwa linahuisha ile roho iliyo na huo uzima. Mungu anapotaka kuhuisha roho yako kwa uzima wake anakupa neno lake lililo na roho ya uzima ndani yake, mchawi naye anapokutamkia maneno ya mauti, roho ya mauti inahuika ndani na kutenda kazi.

Mambo haya mawili yanatuwekea msingi kuelewa ni namna gani basi neno la Mungu linavyoweza kuimarisha roho ya mtu. Mtu ni roho, anayo nafsi na anaishi kwenye nyumba inayoitwa mwili. Kilicho muhimu ni roho kuliko vingine vyote, bali ili roho iweze kufanya kazi vizuri hapa duniani inahitaji mwili na nafsi kama mtafsiri kati ya mwili na roho. Roho inapaswa kushibishwa na mambo ya rohoni na mwili kula vya mwilini. Kwa maana asili ya roho ni roho na asili ya mwili ni udongoni.

Asante na Mungu akubariki. Endelea kufuatilia muendelezo wa somo hili.
NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -1 NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO -1 Reviewed by Unknown on 1:36:00 PM Rating: 5

No comments:

Sora Templates