BREAKING NEWS

[5]

NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU



NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU




Utangulizi

Fahamu Aina ya Ulimwengu Tunaoishi

Ulimwengu huu tunaoishi ni ulimwengu wa shida, adha, mateso, majaribu, uliojaa uovu, dhambi na machafu ya kila aina, biblia inautaja kama “…….dunia hii mbovu iliyopo sasa…..” (Galatia 1:4). Kila kukicha asubuhi, ukigeuka huku na huku, ukisafiri huku na kule, utasikia na kuona ukishuhudia maasi, maovu yanayoendelea ulimwenguni humu, hakika ni mambo ya kutisha. Dunia hii imejaa katika kukosa na kumkana BWANA na katika kugeuka isimtafute Mungu, ikinena jeuri na uasi na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni, hukumu imegeka ikaenda nyuma na haki inasimama mbali sana, maana kweli imeanguka katika njia kuu na kupungua kabisa na unyofu  hauwezi kuingia. Licha ya haya yote yanayoendelea, ndio ulimwengu tunaoishi kwa sasa, na bado Mungu anahitaji tuishi maisha ya ushindi ya kumpendeza.


Hii iko wazi kabisa kwamba shetani ndio chanzo au kwa maneno mengine kwake ndiko yalikoanzia lakini mwanadamu ndiye aliyeruhusu yakapata nafasi na nguvu juu yake mwenyewe na ulimwengu mzima. Kwa mfano biblia inatuarifu kwamba “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakusima katika kweli kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo” (Yoh 8:44). Hii inatuonesha kwamba Ibilisi ndiye chanzo au mwanzilishi wa uongo na uuaji na ndani yake kumejaa huo na mbegu yake uiachilia ndani yao wote wanaoambatana naye. Neno baba maana yake chanzo au mwanzilishi na mmiliki. Mungu ni baba yetu kwa sababu wanadamu wote tuliumbwa kutoka kwake, tunaowaita baba kwa jinsi ya mwili ni kwa sababu tumetokea kwao kwa jinsi ya mwili ndio maana wanasayansi wanasema kibiologia mtoto  ni wa baba na sio wa mama kwa sababu mtoto hatokei kwa mama bali hutokea kwa baba ndio maana hata vinasaba (DNA) vinapimwa kwa baba.


Kwa mantiki hiyo shetani ndiye mwanzilishi wa uongo, uuaji na adha nyingine, na anapofanikiwa kupata umiliki wa watu anapandikiza ile mbegu na hao watu hujikuta kutamani kufanya yaliyo mapenzi ya baba yao au mmiliki wao ambaye ni shetani.


Kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo,  ingawaje shetani ambaye ndiye Ibilisi ndiye chanzo au mwanzilishi wa machafu, maovu, adha, dhambi na maasi, shida na majaribu yote tunayoyajua na tusiyoyajua lakini mwanadamu ndiye aliyeyafungulia mlango na kuyarusu ulimwenguni kufanya kazi na kuwa na nguvu juu yake mwenyewe. 

Biblia inasema “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti, na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu watu wote wamefanya dhambi” (Rum 5:12)   

Kwa hiyo yote tuyaonayo yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu yaliingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja aliyeyaruhusu kuingia. Neno ’iliingia’ linaonesha wazi kwamba dhambi ilitumia mlango uliokuwa tayari kuiruhusu kupita, ikiwa na maana kwamba dhambi haikukutana na kikwazo chochote mlangoni ambacho kingeweza kuzuia kwa hiyo vikwazo viliondolewa na mlinda mlango na kuuacha mlango kuwa wazi na dhambi ikaingia. Ni vizuri kujua hili kwamba wakati wote dhambi iko mlangoni inasubiri kuingia katika ulimwengu wako na kuleta madhara. Mungu alimwambia Kaini “……dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe….” Mwa 4:7


Tukisoma katika Mwanzo 1:26-28 tunaona wazi kwamba Mungu aliyeumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo ndani yake alimpa mwanadamu aliyemuumba kumiliki na kuitawala nchi na vyote vilivyomo ndani yake kama mfalme. Utawala na umiliki huo ulikuwa unalenga uitiisha nchi, bahari na vyote vilivyo ndani yake kwa taratibu na sheria za mbinguni ambazo kwa wazi zingeonesha uhalisia wa tabia na matendo ya  Mungu duniani. Dunia itawaliwe na tabia na matendo ya Mungu ikiwa ni pamoja na upendo na utakatifu na kufanya ulimwengu kuwa mahali sahihi pa kuishi na kustawi. Mungu alikusudia matunda ya mbegu yake yawe ndiyo pekee yanayofahamika na kujulikana ulimwenguni kote, ili kutimiza hazma hii aliiumba sura(tabia) yake ndani ya mwanadamu kabla ya kumpa ufalme ili huyo mwanadamu atakapotawala azae matunda ya sura hiyo.


Lakini tunaona wazi anguko lake lilivyokuwa kubwa kwa huyo mwanadamu baada ya kushindwa kushika na kutii maagizo ya Mungu. Anguko hilo ilibadilisha umiliki wa ulimwengu kutoka kwa mwanadamu kwenda kwa shetani na shetani kuitwa mungu au mkuu wa ulimwengu huu (Yoh 14:30), lakini pia wakati Yesu anajaribiwa, shetani “….akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu na fahari yake, akamwambia haya yote nitakupa, ukinisujudia” (Math 4:8-9), inaonesha wazi kwamba shetani alipata umiliki wa ulimwengu na fahari yake yote kwa sababu asingesema nitakupa kama sio yeye mmiliki lakini pia Yesu hakubishia umiliki huo wa shetani alichokataa ni kusujudia.


Baada ya shetani kupata umiliki wa ulimwengu na fahari yake yote, kazi yake ilikuwa moja tu, kuujaza ulimwengu kwa tabia zake na matendo yake. Maovu, machafu, dhambi na mabaya ya kila namna na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Mfano fikiri pamoja nami wakati wa Nuhu jinsi ambavyo aliweza kuijaza tabia yake ndani ya watu wote wa ulimwengu akapona mtu mmoja tu (Nuhu). Ulimwengu mzima uliambatana na kutenda tamaa za baba yao Ibilisi.

Ni vizuri kuelewa kwa kina aina ya ulimwengu tunayoishi. Shetani baada ya kupata nafasi ya kumiliki huu ulimwengu alifanikiwa kutengeneza mfumo wake ambao watu wanaishi kwa huo na kudumisha utamaduni wake. Watu wakilala na kuamka wako kwenye huo mfumo na utamaduni, kila kizazi kinachotokea ulimwenguni kinazaliwa na kukulia katika huo mfumo na utamaduni ambao unadhibiti na kuratibu mwenendo wa maisha yao na kuamua aina ya maisha yao.


Utamaduni ni kama “vacuum” iliyooandaliwa tayari ambacho watu huzaliwa na kukua ndani yake. Kwa hiyo shetani alitengeneza vacuum/ utamaduni wa ulimwengu ambao watu watazaliwa na kukulia ndani yake. Watu wote tukazaliwa na kukulia katika ulimwengu ulio na mfumo na utamaduni wa maovu, mabaya, makosa, madhambi, magonjwa, adha, shida za kila aina na machafu yote tukayakubali na kuyapa kipaumbele kama yaliyo ya thamani kwetu. Kitu chochote kinabadilika kuwa utamaduni kama kitaonekana na kitakubaliwa na watu wa jamii na kufanywa kuwa sehemu ya maisha katika shughuri za kila siku. Ndivyo ilivyokuwa na ndivyo ilivyo ulimwenguni humu. 

Biblia inazungumza habari za Lutu na wale wageni wawili waliomtembelea kwamba “hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee watu wote waliotoka pande zote. Wakamwambia Lutu, wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu tupate kuwajua” (Mwa 19:4-5). Watu wote wa mji wa Sodoma walizaliwa na kukua katika utamaduni wa uzinzi. Kwao waliona ni jambo jema, wakalikubali na kuona ni sehemu ya maisha yao. Watoto walizaliwa na kukulia katika vacuum ya uzinzi na kuona ni jambo la kawaida kwao. Kwa mfano pia kipindi tulichonacho sasa, imezoeleka kwamba kijana ambaye hajafikia umri wa kuoa au kuolewa haiwezekani akaishi bila kuwa na mpenzi wa jinsia nyingine. Ni utamaduni sasa kwamba kijana ni lazima awe na mpenzi wake hata kama bado hajafikia umri wa kuoa au kuolewa. Watoto wanazaliwa na kukukua katika kawaida hiyo, wakiona ni jambo jema nao wanaliendeleza. Ni hafadhari ya nchi za Afrika, lakini nchi za ulaya na nchi za magharibi ni ukweli mtupu katika jambo hili.


Endelea kufatilia mwendelezo wa Somo Hili
NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU NEEMA YA MUNGU INAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAJARIBU NA KUISHI MAISHA YA USHINDI KATIKA ULIMWENGU HUU Reviewed by Unknown on 5:47:00 PM Rating: 5

No comments:

Sora Templates