BREAKING NEWS

[5]

NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-2



NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-2
Karibu tuendelee na mfululizo wa somo hili la namna ya kuikuza roho yako na kuimarisha. Naamini Mungu amekusudia ujifunze hili somo pamoja nasi ndio maana ukapitia blogu hii. Roho mtakatifu aendelee kukufundisha unapoendelea kusoma na kujifunza.
Tuliishia sehemu kwamba,
Roho inapaswa kushibishwa na mambo ya rohoni na mwili kula vya mwilini. Kwa maana asili ya roho ni roho (Mungu) na asili ya mwili ni udongoni.
Roho ya mtu iliumbwa wa neno la Mungu kutoka kwa Mungu. Vitu vyote pia viliundwa kwa neno la Mungu. Ingawa vitu vyote vilitokea kwa neno kutoka kwa Mungu lakini vilitokea kwa mwelekeo tofauti uliotengeneza asili kutofautiana.
Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe majani; miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema,,,, Mungu akasema “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.’’ Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini, kulingana na aina zake na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Mungu akavibariki akasema, “Zaeni mkaongezeke mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.’’ Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: Wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.’’ Ikawa hivyo. Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wafugwao kulingana na aina zake na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema” (Mwanzo 1:11-12, 20-25)
Ukisoma mistari hii utagundua kwamba ingawa kote Mungu alitamka neno lakini alitamka kwenda sehemu tofauti ambayo ndiyo inatuonesha kwamba kitu kilichoumbwa kimeundwa na nini na kimetokea wapi. Mimea, miche na miti ilitokea katika ardhi, samaki katika maji, wanyama wa kila aina kutoka katika ardhi. Alipotamka kwenda kwenye ardhi, ardhi ikatoa hivyo viumbe, maji yakatoa samaki. Kwa hiyo ingawa viumbe viliumbwa kwa neno la Mungu lakini vina asili ya udongo na maji na ili viweze kustawi vinahitaji udongo na maji na vitu vilivyo na asili yao. Miti, na wanyama inahitaji udongo, samaki wanahitaji maji kuishi.
Mungu alipokuwa anamuumba mwanadamu, alisema neno kama alivyofanya kwa miti, miche, samaki na wanyama lakini kwa mwelekeo tofauti. Wakati huu hakutamka kwenda kwenye ardhi wala maji bali kwenda kwake mwenye na kutoka kwake mwanadamu akatokea.
Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.’’ Kwa hiyo Mungu alimwumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba” Mwanzo 1:26-27.

Kama vile neno la Mungu lilivyoenda katika ardhi, na ardhi ikatoa viumbe hai ndivyo hivyo hivyo lilivyoenda kwa Mungu na Mungua akatoa mwanadamu. Kwa hiyo kama vile mimea na wanyama ilivyo na asili ya udongo (ardhi) ndivyo hivyo hivyo mwanadamu alivyo na asili ya Mungu. Ndiyo maana wanyama na mimea inapokufa inarudi udongoni na mwanadamu akitoka duniani (kufa) anarudi kwa Mungu. Mungu ni Roho (Yoh 4:24) ndiyo maana mwanadamu pia roho iliyo na asili ya Mungu. Ndiyo maana mtu hatakiwi kujidharau hata kama wenzake wanamdharau kwa sabubu ameundwa na vitu alivyoundwa navyo Mungu. Haleluya!
BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7)
Mstari huu unatuonyesha mahali mwili wa mwanadamu ambao ndiyo nyumba ya roho yake ulikotokea. Mungu alifanya mwili kutoka katika mavumbi ya ardhi, kwa maneno mengine ni kwamba asili ya mwili ni mavumbi ya ardhi (udongo). Ndiyo maana mtu anapouacha mwili, mwili hubadilika kuwa udongo katika asili yake. Mungu alimwambia Adamu Kwa jasho la uso wako utakula chakula hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi’’ (Mwanzo 3:19)
Ili mwili uendelee kuwa na nguvu na kuishi vizuri kwa afya unahitaji kushibishwa na vitu vya asili yake yaana ardhi (udongo). Mungu angali akijua hili alimwambia mwanadamu

Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa kwa ajili ya chakula chenu, Cha wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi. Kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.’’ Ikawa hivyo” (Mwanzo 1:29-30)

Ili kuhakikisha mwili unastawi na kunawili, Mungu akamwekea tayari mwanadamu vitu hivyo ili aishi kwa hivyo. Mtu asipokula kwa mda mrefu mwili wake hudhoofika, hukosa nguvu na hatimaye hufa kabisa. Na roho ya mtu ni hivyo hivyo pia. Sasa kilicho muhimu kwa Mungu sio mwili bali roho ya mtu. Kama Mungu anajali mwili wa mwanadamu namna hii si zaidi sana roho yake? Kwa sababu hii, akaweka tayari pia chakula ambacho roho itashiba, kukua, kuongezeka nguvu na kustawi kwa hicho- Neno lake- ambalo linaasili sawa na roho.
Mwili hauwezi kula vitu vya rohoni bali unaweza kuhuishwa na roho yako. Uhai ulio katika roho yako unaambukizwa katika mwili wako, roho yako inapopona na mwili wako unapona. Na roho haiwezi kushibishwa na vitu vya mwilini kwa sababu vina asili tofauti. Na mtu wa asili ya mwilini hawezi kupokea mambo ya rohoni (kwake ni upuuzi) lakini mtu wa rohoni huvipokea.
Kwa hiyo roho ya mtu inahitaji neno la Mungu (hicho ni chakula chake) kama vile mwili unavyohitaji chakula chake (wali, ugali, mihogo, pizza, nyama n.k). Hilo neno la Mungu linaenda kuimarisha roho ya mtu ndani na kumjengea msingi imara ndani yake. Litakiwalo ni kwamba mtu inampasa kusoma neno na kulitafari. Ukila wali baada ya mda unamengenywa na kufyonzwa na kuwa sehemu ya mwili. Ukichunguzwa tumboni hawataona wali tena wala hawataweza kutofautisha kati ya chakula ulichokula na mwili wako. Neno linatakiwa liwe sehemu ya roho yako pia. Unapalitafakari neno sana lile neno linakuwa sehemu ya roho yako.
Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake Yeye ambaye Kwake tutatoa hesabu” (Ebrania 4:12-13)
 Neno la Mungu ndilo liletalo uhai na nguvu ndani ya roho ya mtu na kila wakati mtu huyo akilitafari neno hilo anapata uhai mpya (kuhuishwa) na nguvu mpya. Kwa hiyo nguvu huongezeka rohoni kwa kadiri ya kutafakari neno. Ni Neno la Mungu linalofungua masikio ya ndani (rohoni) ili uweze kusikia vizuri kwa maana “…… kusikia huja kwa neno la kristo” (Warumi 10:17)
Ukweli ni kwamba tunaishi kwenye dunia ambayo inatufanya tuwe kwenye vita vya mara kwa mara bila kupumzika (constant battle) na shetani. Sababu ni kwamba, mara tu mtu anapozaliwa mara ya pili, ingawa anaisha ndani yake (dunia) lakini siyo sehemu yake na anawekewa ndani yake namna ya kuibadiri dunia kwa ufalme wa Mungu. (to effect the earth with the kingdom of God). Kwa hiyo mtu anatakiwa kuwa na mfumo, sheria, taratibu, maagizo na amri tayari ndani yake na nguvu ya kupigana ili kuyadhihirisha hayo. Neno la Mungu ndilo linalotengeza mfumo, sheria, taratibu, maagizo na amri na nguvu inatokea ndani yake.
“ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma (Isaya 55:11)
Tafsiri nyingine ya biblia imeandika hivi;
ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu: Halitanirudia tupu, bali litatimiliza lile nililokusudia na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma. (Isaya 55:11)

Biblia inasema neno la Mungu lina nguvu, hiyo nguvu ndiyo inayofanya kutimizwa kwa kile kinachosemwa na hilo neno. Kwa maneno mengine, neno linapotoka kinywani mwa Mungu linakuwa na kila kinachohitajika ndani yake kufanikisha linalokisema (fully equipped inside, with all it takes to fulfill what it talks about). Neno linafanikiwa kwa sababu lina nguvu ya kutosha kutimiza kusudi lile lilotumwa kulitimiza.
Mtu anatakiwa awe na neno lililo na nguvu ndani yake yakumsaidia kufanikisha kile anachohitaji ikiwamo kushinda vita dhidi ya shetani na mambo yake. Anahitaji nguvu ya kumsaidi kuona anashika sheria ya Mungu, taratibu na amri za Mungu na kuweka mfumo wa ufalme wa Mungu katika ya wanadamu. Hiyo nguvu inatoka ndani ya neno la Mungu.
Mtu haitaji neno tupu (mere word) bali lililo na nguvu ndani yake ili kuweza kupigana vyema na kushinda vita dhidi ya shetani na mambo yake kisha kusimama imara.
Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni…….. Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu (Efeso 6:13-17)
Neno la Mungu ni silaha, na kwenye mistari hii linatajwa likiwa na kazi mbili kuu, kujilinda na kushambulia. Biblia inasema “…mmejifunga kweli….” Kweli ni neno la Mungu (Yoh 17:17). Na anaposema kiunoni anazungumzia habari ya ‘nafsi’ inayoundwa na fikra, mawazo na hisia. Nafsi ndiyo inayosaidia kutengeneza msimama ndani ya mtu. Kwa kiyo anaposema “….mmejifunga kweli kiunoni…” alikuwa anamaanisha kuifunga nafsi (fikra na mawazo) katika neno la Mungu. Nafsi ikubaliane na neno la Mungu. Hii inamfanya mtu kuwa amesimama imara sehemu au uwanja sahihi kupigana.  Neno la Mungu ni upanga kwa ajili ya kushambulia adui. Kwa hiyo mtu anahiji neno la Mungu kwa ajili ya kumuimarisha na kumlinda na kwa ajili ya kumshambulia adui awapo vitani. La zaidi ni kwamba silaha zote zinazotajwa katika Efeso 6, ni silaha moja tu kwa ajili ya kushambulia na kumpiga adui, nayo ni neno la Mungu. Nyingine zote ni kwa ajili ya kujilinda (Protection)
Kwa hiyo mtu anaongezeka kuwa hodari katika vita kwa kadiri anavyopata mda mwingi wa kusoma, kusikiliza na kutafakari neno la Mungu kila siku. Neno linafyonzwa kuingia rohoni mwa mtu kwa kutafakari hilo neno pamoja na Roho mtakatifu. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kukufunulia yaliyofichwa ndani ya kilo neno, na huwezi kuyapata hayo isipokuwa wakati wa kutafakari hilo neno. Kwa kutafakari hilo neno ndipo unapopata ufahamu sahihi wa kufanya mambo. Huwezi pia kufanya sawa sawa na hilo neno isipokuwa umepata nafasi ya kutafakari hilo neno na kupata ufahamu wa namna wa kulifanya na nguvu ya kulifanya sahihi.
“Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, Bali yatafakari maneno yake mchana Na usiku, upate kuangalia kutenda sawa sawa Na maneno yote yaliyoandikwa humu; maana ndipo utakapofanikisha njia yako, kisha ndipo utapapostawi sana” (Yoshua 1:8)
Kutafakari neno, kunampa mtu ufahamu na nguvu ya kutenda sawa sawa na hilo neno na kufanikisha njia yake. Ataendelea kustawi vizuri kwa kadiri anapopata mda mwingi kutafakari hilo neno. Inapasa kuendelea na kutafakari hilo neno mpaka anapopata ufunuo kwa kuvuviwa na Roho mtakatifu na anapoendelea kutumia ufahamu huo anazidi kuimarika rohoni. Narudia tena, anapoendelea kuutumia (practice) huo ufahamu. Yesu katika Marko 4:24 akiwa na watu,
Akawaambia, angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa” (Marko 4:24)
Kwa tafsiri ya kiingereza (Amplied Bible) inasomeka hivi,
And He said to them, Be careful what you are hearing, The measure [of thought and study] you give [to the truth you hear] will be the measure [of virtue and knowledge] that comes back to you and more [besides] will be given to you who hear
Kwa tafsiri isiyo rasmi Ikiwa na maana “Akawaambia, angalieni msikialo, kipimo kile (cha tafakari na kujifunza) mkipimacho kwa kweli muisikiayo, kitakuwa ndicho kipimo cha (nguvu na maarifa) kitakachowajilia, na zaidi mtazidishiwa kwenu ninyi mnaosikia”
Mtu akitumia mda kidogo kutafakari atakuwa na ufahamu na nguvu kidogo, bali kwake yeye anayetumia mda mwingi kutafari kwake yeye hupewa vingi. Na kweke yeye asiyetaka kutafakari neno, anahesabiwa amekataa maarifa, kwake yeye maangamizo ni hakika na BWANA humkataa yeye pamoja na watoto wake.
Biblia inasema Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi name nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako (Hosea 4:6)
Basi neno la kristo na likae kwa wingi moyoni ili kuweza kufanikiwa.
Mungu akubariki, andelea kufatilia mfululizo wa somo hili.

NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-2 NAMNA YA KUKUZA NA KUIMARISHA ROHO YAKO-2 Reviewed by Unknown on 6:34:00 PM Rating: 5

No comments:

Sora Templates